Hizbullah: Lebanon haitatawaliwa na Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i2059-hizbullah_lebanon_haitatawaliwa_na_saudia
Harakati ya Hizbullah imeonya kuwa Lebanon kamwe haitakuwa chini ya mamlaka ya Saudi Arabia licha ya kuwepo mashinikizo ya ufalme huo kwa maafisa wa Lebanon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 27, 2016 13:23 UTC
  • Hizbullah: Lebanon haitatawaliwa na Saudia

Harakati ya Hizbullah imeonya kuwa Lebanon kamwe haitakuwa chini ya mamlaka ya Saudi Arabia licha ya kuwepo mashinikizo ya ufalme huo kwa maafisa wa Lebanon.

"Lebanon haitakuwa chini ya utawala wa Saudi au dola lingine lisilo Saudia", amesema Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah Sheikh Naim Qassem.

Alitoa kauli hiyo jana Ijumaa kufuatia hatua ya Saudi Arabia kukata msaada wa kijeshi wa dola bilioni nne. Saudia imekata msaada huo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Gibran Bassil kukataa kuomba msamaha baada ya kupinga muswada uliotayarishwa na ufalme huo dhidi ya Iran katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Aidha Saudia imeyawekea vikwazo mashirika manne ya Lebanon na watu watatu wanaodaiwa kuwa na mfungamano na Hizbullah. Wakuu wa Riyadh pia wamewataka Wasaudi waondoke Lebanon huku kukiwa na tetesi kuwa raia wengi wa Lebanon wanaofanya kazi Saudia watatimuliwa.

Sheikh Naim Qassim amesema Saudi ndiyo inayopaswa kuiomba Lebanon msamaha kwa hatua zake za uhasama. Amesema kwa muda mrefu sasa Saudia imekuwa ikitafuta kisingizio cha kuihujumu Lebanon na Hizbullah na sasa inatumia mwanya uliojitokeza.

Mawaziri kadhaa wa Lebanon wamesema nchi hiyo katu haitaiomba Saudia msamaha huku Waziri Mkuu, Tammam Salam akitoa wito kwa nchi hiyo kuungana kukabiliana na mashinikizo ya Saudia. Habari nyingine zinasema Saudia pia imekata misaada ya kijeshi kwa Lebanon baada ya mwanamfalme wa ukoo wa Aal Saud kuendelea kushikiliwa Lebanon baada ya kukamatwa akiwa na dawa za kulevya katika uwanja wa ndege wa Beirut mwezi Oktoba mwaka jana. Abdul-Mohsen al-Waleed Al Saud alipatikana na tani mbili za mihadarati aina ya amphetamine captagon.

Sababu nyingine ya hasira za Saudia ni ushindi wa wapignaji wa Hizbullah dhidi ya magaidi wanaopata himaya na misaada ya Saudia nchini Syria.