Hizbullah: Hatuwezi kuiomba Saudia msamaha
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah imeukosoa utawala wa Saudi Arabia kwa kula njama ya kuitumbukiza Lebanon katika mzozo wa ndani na kuongeza kuwa katu haiwezi kuiomba msahama serikali ya Riyadh kwa kusema ukweli.
Sheikh Nabil Qaouk, Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la harakati hiyo amesema muda sio mrefu utawala wa Aal-Saud utatambua kuwa ulipiga mahesabu mabaya ya kujaribu kuingilia masuala ya ndani na uhuru wa kujitawala wa Lebanon. Hii ni katika hali ambayo, Hizbullah imeonya kuwa Lebanon kamwe haitakuwa chini ya mamlaka ya Saudi Arabia licha ya kuwepo mashinikizo ya ufalme huo kwa maafisa wa Lebanon. Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sheikh Naim Qassim amesema Lebanon haitakuwa chini ya utawala wa Saudia au dola jingine lisilo Saudia. Sheikh Qassim ametoa kauli hiyo kufuatia hatua ya Saudi Arabia kutangaza kuikatia Lebanon msaada wa kijeshi wa dola bilioni nne. Saudia imekata msaada huo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Gibran Bassil kukataa kuomba msamaha baada ya kupinga muswada uliotayarishwa na ufalme huo dhidi ya Iran katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Aidha Saudia imeyawekea vikwazo mashirika manne ya Lebanon na watu watatu wanaodaiwa kuwa na mfungamano na Hizbullah. Wakuu wa Riyadh pia wamewataka Wasaudi waondoke Lebanon huku kukiwa na tetesi kuwa raia wengi wa Lebanon wanaofanya kazi Saudia watatimuliwa. Sheikh Naim Qassim amesema Saudia ndiyo inayopaswa kuiomba Lebanon msamaha kwa hatua zake za uhasama. Amesema kwa muda mrefu sasa Saudia imekuwa ikitafuta kisingizio cha kuihujumu Lebanon na Hizbullah na sasa inatumia mwanya uliojitokeza.