Assad: Kukombolewa Aleppo ni ushindi kwa Syria, Iran na Russia
Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema kukombolewa kikamilifu mji wa kistratejia wa Aleppo (Halab), kaskazini magharibi mwa nchi ni ushindi mkubwa sio tu kwa taifa hilo, bali pia kwa Iran na Russia.
Rais Assad ameyasema hayo leo katika mazungumzo yake na Hossein Jaberi Ansari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kubainisha kuwa, kukombolewa Halab pia ni pigo kwa nchi ambazo ni maadui wa taifa la Syria ambazo zinatumia ugaidi kufikia malengo na maslahi yao.
Rais Bashar Assad wa Syria ameongeza kuwa, ushindi huo ni hatua kubwa ya kuelekea kumaliza vita na harakati za kigaidi katika nchi hiyo.
Kwa upande wake, Hossein Jaberi Ansari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayesimamia masuala ya nchi za Kiarabu na Afrika amempa habari Rais wa Syria kuhusu jitihada za kidiplomasia zinazonuia kutokomeza ugaidi nchini Syria, yakiwemo mazungumzo ya pande tatu kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Russia na Uturuki.
Kadhalika Ansari ameashiria uhusiano wa kistratejia kati ya Tehran na Damascus na kusema kuwa, uhusiano huo wa pande mbili umesaidia kuzima njama za maadui.
Huku hayo yakiarifiwa, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imesema kuwa, shughuli ya kuwahamisha raia na wapiganaji waliosalia katika mashariki mwa mji wa Aleppo inakamilika katika muda wa masaa machache yajayo, kwa kutumia mabasi 40 na mamia ya magari ya kibinafsi.
Usiku wa kuamkia Disemba 13, wakazi wa mji huo walitoka mabarabarani kwa shangwe, vifijo na vigelegele, baada ya kupokea habari za kukombolewa kikamilifu mji huo, uliokua moja ya ngome kuu za wanachama wa magenge ya kigaidi nchini Syria.