Jaberi Ansari: Mazungumzo ya Astana kuhusu Syria yanaendelea kupiga hatua
Mkuu wa ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya Astana kuhusu mgogoro wa Syria amesema mazungumzo hayo yanaendelea kupiga hatua.
Hussein Jaberi Ansari, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria mwenendo wa mazungumzo yaliyofanywa baina ya ujumbe wa Iran na wawakilishi wa Russia na Uturuki kwa ajili ya kuendeleza suluhu na amani nchini Syria na kueleza kwamba ufuatiliaji wa hati za maafikiano ya kuendeleza usitishaji vita ni miongoni mwa ajenda za duru ya tatu ya mazungumzo ya amani ya Syria yanayoendelea katika mji mkuu wa Kazkhstan, Astana.
Jaberi Ansari ameongeza kuwa katika duru hii ya tatu ya mazungumzo, wawakilishi wa nchi hizo watachunguza pia hati tatu zinazohusiana na uteguaji mabomu na kubadilishana mateka na kuziwasilisha kwa pande husika za mgogoro wa Syria.
Jana Jumanne ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulifanya mazungumzo katika nyakati tofauti na jumbe za Russia na Uturuki.
Mazungumzo rasmi ya duru ya tatu kuhusu mgogoro wa Syria yanatazamiwa kuanza leo Jumatano kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa Iran, Russia na Uturuki pamoja na mwakilishi wa Jordan, Bashar al-Jaafari anayeiwakilisha serikali ya Syria na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa.
Duru ya kwanza ya mazungumzo ya amani ya Syria ya Astana ilifanyika tarehe 23 na 24 Januari na ile ya pili ilifanyika tarehe 15 na 16 Februari katika mji mkuu huo wa Kazakhstan.
Hivi karibuni Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitangaza kuyatambua na kuyaunga mkono mazungumzo ya Astana kwa ajili ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria huku likitoa mwito wa kuendelea mazungumzo hayo ambayo yanafanyika kwa ubunifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikishirikiana na Russia na Uturuki.
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa mashambulizi makubwa ya makundi ya kigaidi yanayosaidiwa na Saudi Arabia, Uturuki, Qatar, Marekani na Israel dhidi ya serikali halali ya nchi hiyo.../