Netanyahu: Tutaendelea kuwapa matibabu magaidi wa Syria
Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel amesema Tel Aviv itaendelea kuwapa matibabu magaidi wanaojeruhiwa katika harakati zao za kujaribu kuingusha serikali halali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria.
Sambamba na kutoa matamshi hayo ya kifidhuli, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine ameipongeza serikali ya Marekani kwa kuishambulia Syria.
Akizungumza kabla ya kuanza kikao cha Baraza la Mawaziri katika mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu hapo jana, Netanyahu amesisitiza kuwa Israel itaendelea kuwatibu magaidi wa Syria, kama njia moja ya Tel Aviv ya kuunga mkono kile alichokitaja kuwa 'juhudi za kibinadamu'.
Inaarifiwa kuwa, magaidi hao hasa wa kundi la ISIS au Daesh na wale wa Jabhatu Nusra, tawi la al-Qaeda, wamekuwa wakipata matibabu katika hosptili za jeshi la Israel katika miinuko ya Golan.
Masaa machache baada ya Marekani kuvurumisha makombora dhidi ya Syria siku chache zilizopita, Netanyahu aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kuwa: "Nampongeza Rais Donald Trump kwa 'ujasiri' wa kuagiza kutekelezwa mashambulio hayo dhidi ya Syria."
Alfajiri ya Ijumaa iliyopita, Marekani ilifyatua makombora 59 ya Tomahawk yaliyolenga kituo cha jeshi la anga cha al- Shayrat kilichoko mkoani Homs magharibi mwa Syria, yakitokea kwenye manowari za jeshi la US zilizoko kwenye maji ya Bahari ya Mediterania.