Magaidi wakamatwa na silaha za Israel nchini Syria
Vyombo vya usalama vya nchini Syria vimetangaza kuwa vimekamata magaidi kadhaa waliokuwa na silaha za utawala wa Kizayuni wa Israel nchini humo.
Televisheni ya al Alam imetangaza kuwa, askari wa ulinzi wa wananchi katika mkoa wa Suwayda wa kusini mwa Syria wamekamata shehena kubwa ya silaha za kila aina za utawala wa Kizayuni wa Israel mikononi mwa magaidi wanaofanya mauaji nchini Syria.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, magaidi hao walikuwa wako katika harakati za kupeleka silaha hizo kwa magaidi wenzao walioko kwenye eneo la al Badiya la mashariki mwa Syria.
Hii si mara ya kwanza kubainika kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unayasaidia magenge ya kigaidi nchini Syria kwa mali na kwa silaha.
Msaada wa Israel kwa magaidi wa Syria ni mkubwa na ni wa wazi kiasi kwamba, wakati magaidi hao wanapojeruhiwa katika mapigano na wanajeshi wa Syria huwa wanapewa matibabu na utawala wa Kizayuni. Uungaji mkono wa Israel kwa magaidi wa Syria ni mkubwa kiasi kwamba hata Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni huwatembelea magaidi hao hospitalini.