May 26, 2017 14:13 UTC
  • Wanaharakati 14 wahukumiwa kifo kwa kuandamana Saudia

Mahakama moja nchini Saudi Arabia imewahukumu adhabu ya kifo wanaharakati 14 kwa kushiriki maandamano katika eneo la Qatif.

Kanali ya televisheni ya al-Manar ya Lebanon imesema Mahakama ya Juu ya Saudia mjini Riyadh imewahukumu vijana hao wanaharakati adhabu ya kifo kwa kushiriki maandamano ya amani dhidi ya utawala wa Aal-Saud, katika eneo la Qatif, Mkoa wa Mashariki.

Inaarifiwa kuwa, vyombo vya usalama viliwatesa na kuwanyanyasa wanaharakati hao wakati wa kusikilizwa kesi zao, ili kuwashurutisha wakiri kwamba wamefanya makosa ambayo wanatuhumiwa kuhusika nayo.

Hukumu hiyo imetolewa chini ya Sheria ya Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2014, ambayo imezusha makelele mengi kutoka mashirika mbali mbali ya kutetea haki za binadamu.

Sheikh Nimr aliuawa na watawala wa Aal-Saud mwaka jana

Mapema mwezi huu, Ben Emmerson, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa aliutaka utawala wa Riyadh kutotumia sheria hiyo kandamizi dhidi ya watu wanaotumia uhuru wao wa kukusanyika, kijieleza na kukosoa.

Siku ya Jumatano, wanajeshi wa Saudia waliendeleza hujuma mjini al-Awamiya mashariki mwa nchi kwa kudondosha mabomu katika eneo hilo, lenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Watawala wa Saudia wanataka kukiharibu kijiji cha al-Masourah kilichoko katika mji wa al-Awamiya, alikozaliwa Sheikh Nimri Baqir an-Nimr, mwanazuoni mkubwa wa Waislamu wa Kishia aliyeuawa kwa kukatwa kichwa na utawala huo mwaka jana. 

 

Tags