Mwandishi wa Algeria: Saudia ni silaha inayotumiwa na Marekani kuwahujumu Waislamu
Mwandishi maarufu wa nchini Algeria Haddat Hizam, amesema kuwa kinyume na madai yanayotolewa, Saudia si tu kwamba haina na nafasi yoyote yenye maslahi katika eneo, bali ni nyenzo bora inayotumiwa na Marekani kuwalenga Waislamu.
Hizam ameyasema hayo leo katika makala aliyoyaandika kwenye gazeti la al-Fajr la nchi hiyo na kuongeza kuwa, utawala wa kifalme wa Saudia kila siku unatumia mamia ya mabomu kuwashambulia watoto wadogo na wanawake wa Yemen na kuharibu miundombinu ya taifa hilo masikini la Kiarabu, kwa lengo la kutaka kuirejesha madarakani nchini humo serikali kibaraka wake na Marekani.
Haddat Hizam Amefafanua kuwa, baadhi ya vyombo vya habari vinashiriki katika mauaji ya Saudia katika kutenda jinai kubwa nchini Yemen kupitia upotoshaji habari kuhusiana na kadhia ya Yemen. Akibainisha kwamba Saudia ni nyenzo bora ya Marekani dhidi ya mataita ya Kiarabu na Kiislamu, mwandishi huyo wa Algeria ameashiria matamshi ya Rais Donald Trump wa Marekani aliyoyatoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa mwaka jana nchini humo kwamba, ili kuendelea kupata ulinzi wa Washington Saudia inatakiwa kutoa theluthi tatu ya utajiri wake kuipa Marekani, ambapo baadaye rais huyo alifanya safari ya hivi karibuni mjini Riyadh na kusaini mkataba wa mamia ya mabilioni ya Dola kwa maslahi ya Marekani.
Ni zaidi ya miaka mitatu sasa ambapo Saudia inaendesha vita na jinai kubwa dhidi ya Yemen kwa kushirikiana na Marekani, Israel na mataifa mbalimbali ya Kiarabu na Kimagharibi.