Rais wa Syria: Tumezishinda njama za madola ya Magharibi
Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema kuwa pamoja na kwamba taifa la Syria limepata hasara kubwa katika vita vya kupambana na ugaidi, lakini njama za madola ya Magharibi zimefelishwa nchini humo.
Rais Bashar al-Assad ameyasema hayo katika kongamano la Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria ambapo sambamba na kuashiria malengo machafu ya maadui ya kuanzisha vita ndani ya nchi hiyo amesema kuwa, kuidhibiti Syria kuna maana ya kuidhibiti Mashariki ya Kati yote. Ameongeza kuwa, mtu yeyote anayedhibiti eneo la Mashariki ya Kati, huwa mwenye taathira kubwa katika uga wa kimataifa. Rais Bashar al-Assad ameshukuru misaada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nchi yake katika vita dhidi ya ugaidi na kadhalika miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei na kueleza kwamba, mara zote Iran imekuwa ikiisaidia Syria kwa misaada mingi ya kiuchumi, kijeshi na kisiasa.
Huku akibainisha kwamba gharama za kusimama imara ni ndogo kuliko gharama ya kusalimu amri, amesema kuwa Russia, Iran na Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon zimekuwa na nafasi kubwa katika kufanikisha muqawama wa Syria na kusonga kwake mbele katika uwanja wa vita. Hayo yanajiri katika hali ambayo jeshi la Syria kwa kushirikiana na harakati ya muqawama ya Hizbullah limeendelea kupata mafanikio makubwa katika vita dhidi ya magaidi wakufurishaji wanaopata uungaji mkono wa Marekani, Saudia, Israel, Uturuki na baadhi ya nchi za eneo na nje ya eneo.