Sisitizo la Syria la kutokuwa na silaha za kemikali
Katika kujibu madai ya kamisheni ya uchunguzi inayosimamiwa na Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, kuhusiana na utumiwaji wa silaha hizo na serikali ya Syria, Damascus imetangaza kuwa haina silaha za namna hiyo.
Hussam Eddin Ala, mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva amenukuliwa akisema katika ujumbe alioutoa kwa Mkuu wa Baraza la Haki za Binaadamu la umoja huo ambapo sambamba na kusisitiza kuwa Damascus haina silaha za namna hiyo amefafanua kuwa, utumiwaji wa silaha za kemikali ni kitendo cha jinai. Mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva ameashiria kuwa, sambamba na kuwepo indhari za mara kadhaa za serikali ya Syria kuhusiana na mienendo isiyoridhisha ya kamisheni hiyo ya UN, lakini bado inaendeleza tuhuma zake za uongo dhidi ya taifa la Syria.
Lengo la kutolewa madai hayo bandia dhidi ya Syria kupitia kamisheni na mashirika ya Umoja wa Mataifa, ni kuandaa mazingira yenye lengo la kuyazatiti zaidi makundi ya kigaidi kwa silaha hizo hatari kwa minajili ya kuzuia kushindwa kikamilifu magenge hayo nchini Syria. Aidha lengo la kundi la Daesh la kutumia zaidi silaha za kemikali, ni kuibua hali ya wasi wasi mkubwa kati ya raia wa Syria ili kuwazuia kutoa ushirikiano wao kwa serikali. Katika uwanja huo, Kamal Jafa, mtaalamu wa masuala ya kijeshi na stratijia wa nchini Syria amesema: "Tuhuma za hivi karibuni dhidi ya serikali na jeshi la Syria, zimetolewa kwa malengo mawili ambayo ni kutekeleza stratijia za kisiasa na kijeshi kwa ajili ya makundi ya kigaidi." Mwisho wa kunukuu.
Katika mazingira hayo, nchi waungaji mkono wa makundi ya kigaidi kama vile serikali za Magharibi na baadhi ya serikali za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, hazipo tayari kukomesha uungaji mkono wao huo kwa magenge hayo. Kivitendo zimekuwa zikiyapatia moja kwa moja makundi hayo zana za kijeshi zikiwemo pia silaha za kemikali. Hii ni katika hali ambayo waungaji mkono hao wa ugaidi nchini Syria, wamekuwa wakifanya udanganyifu kwa lengo la kupotosha ukweli wa kile kinachoendelea nchini humo. Ili kufanikisha mpango wao huo, madola hayo yanayatumia mashirika tofauti ya kuzuia kuenea silaha za kemikali nchini Uholanzi kwa ajili ya kuishinikiza serikali ya Damascus sambmba na kuchukua maamuzi yaliyo dhidi ya serikali hiyo. Huku serikali ya Syria ikiwa inakabiliwa na njama za tuhuma za Wamagharibi kupitia maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, silaha zote za kemikali za taifa hilo la Kiarabu tayari zimekwishakabidhiwa kwa taasisi hizo za kuzuia kuenea kwa silaha za kemikali ambapo hata Umoja wa Mataifa pia umekiri juu ya ushirikiano chanya wa serikali ya Damascus kuhusiana na suala hilo.
Kuhusiana na suala hilo Dmitry Babich, mmoja wa wataalamu wa masuala ya kisiasa na kijeshi wa Russia anasema: "Kwa sasa Syria haina silaha za kemikali na tuhuma zinazotolewa kuilenga serikali ya nchi hiyo zinajiri kupitia njama za kila upande dhidi ya taifa hilo la Kiarabu. Hata Shirika la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kemikali mwaka 2013 lilipewa zawadi ya Nobel kutokana na hatua yake ya kuondoa silaha zote za Syria." Mwisho wa kunukuu. Misimamo ya kugongana ya asasi za kimataifa zikiwemo taasisi tofauti za Umoja wa Mataifa kuhusiana na mgogoro wa Syria, inabainisha namna ambavyo misimamo hiyo ilivyoathiriwa na mashinikizo ya madola ya Magharibi katika uwanja huo. Matukio ya kimataifa yanathibitisha kwamba, mafanikio mtawalia yanayoshuhudiwa katika uga wa operesheni na katika uwanja wa vita ambayo yanajiri kwa maslahi ya serikali ya Syria, ndiyo yamepelekea madola hayo kunzisha njama na propaganda dhidi ya serikali ya Damascus.