Oct 14, 2017 08:08 UTC
  • ADHRB: Saudia, Bahrain na Kuwait zinaongoza kwa kunyonga wapinzani

Jumuiya ya Demokrasia na Haki za Binadamu ya Bahrain (ADHRB) imetangaza kuwa, hukumu za vifo dhidi ya wapinzani zimeongezeka sana katika nchi tatu za Saudi Arabia, Bahrain na Kuwait.

Taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo imelaani hukumu za vifo zinazotolewa kwa wingi katika nchi tatu za Saudi Arabia, Bahrain na Kuwait na kutoa wito wa kusitishwa mara moja utekelezaji wa hukumu hizo. 

Mkurugenzi wa Jumuiya ya Demokrasia na Haki za Binadamu ya Bahrain (ADHRB), Hussein Abdullah amesema inasikitisha kuona kwamba, adhabu ya kifo inatumika katika baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi dhidi ya wapinzani wa kisiasa kwa kadiri kwamba, katika nchi za Saudi Arabia na Bahrain adhabu hiyo ya kifo inatumiwa kama silaha ya kisiasa dhidi ya wanaharakati na wapinzani wa serikali baada ya silaha ya mateso na kufungwa jela kinyume cha sheria na taratibu. 

Saudi Arabia na Bahrain zinaongoza Ghuba ya Uajemi kwa kunyonga wapinzani

Huissein Abdullah ameongeza kuwa, utekelezaji wa hukumu ya kifo katika nchi za Saudia, Bahrain na Kuwait unafanyika kinyume cha sheria na kusisitiza kuwa, idadi kubwa ya watu wanaosubiri adhabu ya kifo si kwa sababu ya jinai au makosa waliyofanya bali ni kutokana na kutetea haki zao zinazotambuliwa kimataifa.

Ripoti iliyotolewa na Jumuiya ya Demokrasia na Haki za Binadamu ya Bahrain (ADHRB) imesema kuwa: Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa zaidi ya watu walionyongwa duniani na kwamba katika miaka mitatu iliyopita zaidi ya raia mia moja wamekuwa wakinyongwa kila mwaka nchini humo.  

Tags