Marekani yakiri magaidi wanatumia silaha za kemikali Syria
Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kwa mara ya kwanza imekiri kwamba, magaidi wanatumia silaha za kemikali huko Syria.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia Jenerali Igor Konashenkov amesema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kukiri kuwa kundi la kigaidi kwa jina la Tahrir al Sham si tu kuwa linamiliki silaha za kemikali bali limetumia silaha hizo.
Jenerali Konashenkov ameongeza kusema kuwa, kabla ya hapo Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ililituhumu jeshi la Syria kuwa limefanya mashambulizi ya kemikali.
Kundi la kigaidi la Tahrir al Sham lina mfungamano na kundi la kigaidi la Jabhatul Nusra linalofanya hujuma katika mkoa wa Idlib huko Syria huku likitumia silaha za aina mbalimbali zikiwemo za kemikali.
Weledi wengi wa mambo wanaitaja hatua ya kutuhumiwa serikali ya Syria kuwa imetumia silaha za kemikali nchini humo kuwa ni katika juhudi za kuzipotosha fikra za walimwengu na kuficha uhakika wa mambo kufuatia ushindi wa hivi karibuni wa jeshi la Syria katika vita dhidi ya magaidi nchini humo.
Tarehe saba mwezi Aprili mwaka huu Marekani iliituhumu serikali ya Syria kuwa ilitumia silaha za kemikali katika eneo la Khan Sheikhun kusini mwa mkoa wa Idlib magharibi mwa nchi hiyo na kisha ikakishambulia kwa makombora 59 kituo cha jeshi la anga huko al Shairat mkoani Homs. Kituo hicho ni ngome kuu ya mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi ya Daesh na Jabhatul Nusra huko Syria.