Faili la jinai za Imarati dhidi ya Yemen lafunguliwa ICC
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36909-faili_la_jinai_za_imarati_dhidi_ya_yemen_lafunguliwa_icc
Shirika moja la kutetea haki za binadamu limewasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, likiituhumu nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa imetenda jinai za kivita ukishirikiana na Saudi Arabia dhidi ya Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 28, 2017 04:14 UTC
  • Faili la jinai za Imarati dhidi ya Yemen lafunguliwa ICC

Shirika moja la kutetea haki za binadamu limewasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, likiituhumu nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa imetenda jinai za kivita ukishirikiana na Saudi Arabia dhidi ya Yemen.

Shirika hilo linalofahamika kama Arab Organization for Human Rights (AOHR) lenye makao makuu yake mjini London linaituhumu Imarati kuwa imetenda jinai za kibinadamu dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen.

Joseph Breham, mmoja wa mawakili wa shirika hilo amesema UAE imekuwa ikitumia mabomu yaliyopigwa marufuku ya vishada sambamba na kuwakodisha mamluki kuwaua na kuwatesa raia wa Yemen.

ICC inatazamiwa kuamua iwapo itaagiza kuanzishwa uchunguzi wa jinai hizo au la, kwa kutilia maanani kuwa Imarati sio nchi mwanachama wa Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi.

Sehemu ndogo ya hujuma za Saudia, Imarati na waitifaki wao dhidi ya Yemen

Saudia kwa uungaji mkono wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, Imarati na baadhi ya nchi za Kiarabu, ilianzisha mashambulizi ya kikatili ya pande zote dhidi ya wananchi wa Yemen mwezi Machi 2015, ambapo watu zaidi ya 12 elfu wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.

Hata hivyo muqawama wa wananchi Waislamu wa Yemen umewatumbukiza kwenye kinamasi kikubwa wavamizi hao ambao hivi sasa wanaanza kugombana wao kwa wao.