Misri yamuonya Trump dhidi ya kuvuruga mambo Mashariki ya Kati
Rais Abdulfattah al-Sisi wa Misri amemtahadharisha mwenzake wa Marekani Donald Trump dhidi ya kuhamishia ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi mji mtukufu wa Quds, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Taarifa ya Ofisi ya Rais mjini Cairo imesema kuwa, Sisi aliyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Trump jana Jumanne, ambapo alimueleza kinagaubaga kuwa: Hatua za aina hii zitafifiza jitihada za kupatikana amani Mashariki ya Kati.
Rais wa Misri amesema msimamo wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ni kuhakikisha kuwa mji wa Quds Tukufu (Jurasalem) unalindwa katika fremu ya sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Trump anatazamiwa hii leo kuutambua rasmi mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala ghasibu wa Israel na kuhamishia ubalozi wa nchi hiyo katika mji huo kutoka Tel Aviv.
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeonya kuwa, kuhamishiwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi mji mtukufu wa Quds hakutakuwa na natija nyingine ghairi ya kuibua ghasia na kuvuruga zaidi hali ya mambo.
Miongoni mwa shakhsia wanaopinga azma hiyo ya Trump ni Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Kiongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson na mwenzake wa Ulinzi Jim Mattis .