Wapalestina waandamana katika "Ijumaa ya Ghadhabu" dhidi ya Trump
Raia wa Palestina leo Ijumaa wamefanya maandamano katika ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu chini ya anwani "Ijumaa ya Hasira" ili kulalamikia na kupinga hatua ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuutangaza mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa Israel.
Wananchi wa Palestina wamekabiliana na askari jeshi wa utawala wa Kizayuni huko Bait Laham na katika kituo cha upekuzi cha Qalandia huko kaskazini mwa mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu katika maandamano hayo ya Ijumaa ya Ghadhabu. Wanajeshi wa Israel waliwafyatulia risasi wafanya maandamano hao wa Kipalestina.
Ripoti zinasema kuwa, askari wa Israel wamewaua Wapalestina wanne katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza na kujeruhi makumi ya kwa risasi.
Wananchi wa Palestina pia walifanya maandamano mengine katika maeneo ya karibu na Msikiti wa al Aqsa baada ya Swala ya Ijumaa hii leo. Utawala haramu wa Israel umechukua hatua kali za kiusalama huko Quds khususan kandokando ya Msikiti wa al Aqsa na katika kitongoji cha Babul Aamud.
Maandamano hayo ya Ijumaa ya Hasira ya kuihami Quds yamefanyika katika maeneo mengine ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ikiwemo huko Ramallah na al Khalil na katika Ukanda wa Ghaza.
Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza leo kuwa, Wapalestina zaidi ya 2700 wajeruhiwa hadi kufikia sasa tangu kuanza Intifadha ya hivi karibuni ya kuihami Quds inayokaliwa kwa mabavu.