Marekani, chanzo cha kuzidi kuwa mbaya hali ya Ukanda wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i39697-marekani_chanzo_cha_kuzidi_kuwa_mbaya_hali_ya_ukanda_wa_gaza
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA limesema katika radiamali yake kwa hatua ya Rais wa Marekani iliyo dhidi ya Palestina kwamba, uamuzi wa Donald Trump wa kuipunguzia misaada taasisi hiyo utashadidisha hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 30, 2018 23:51 UTC
  • Marekani, chanzo cha kuzidi kuwa mbaya hali ya Ukanda wa Gaza

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA limesema katika radiamali yake kwa hatua ya Rais wa Marekani iliyo dhidi ya Palestina kwamba, uamuzi wa Donald Trump wa kuipunguzia misaada taasisi hiyo utashadidisha hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Mgomo wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Gaza wakilalamikia uamuzi wa Rais wa Marekani wa kuwapunguzia misaada Wapalestina ulipelekea juzi Jumatatu kufungwa shule, kliniki za kitiba na vituo vya ugawaji bidhaa za chakula. Washiriki wa mgomo huo wakiwa wamebeba mabango na maberamu waliandamana kuelekea katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Gaza wakitangaza kuwa, kupunguzwa misaada ya Marekani kwa UNRWA kutashadidisha hali mbaya ya kibinadamu katika eneo hilo.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA linaendesha shule 278 katika Ukanda wa Gaza na kuna takribani wanafunzi laki tatu wanaosoma katika skuli hizo.

Nembo ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA

Wiki iliyopita, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ilitangaza kusitisha awamu mbili za misaada ya kifedha ambayo ilikuwa imetengewa mipango ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA. Kwa mujibu wa tangazo hilo zaidi ya dola milioni 100 zimesitishwa. 

Kuna zaidi ya Wapalestina milioni tano ambao ni wakimbizi na familia zao zipo katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati wakiwa chini ya usimamizi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA. Utawala wa Kizayuni wa Israel nao, mwaka 2006 ulianza kulizingira kila upande eneo la Ukanda wa Gaza na umekuwa ukizuia kuingia katika eneo hilo aina yoyote ile ya misaada ya kibinadamu. Sambamba na hatua hizo, uungaji mkono wa baadhi ya madola ya Magharibi hususna Marekani kwa utawala ghasibu wa Israel nao umekuwa ukiupa kiburi zaidi utawala huo cha kuendeleza jinai zake.

Siasa za kiuhasama na chuki za Marekani dhidi ya Wapalestina zimechukua mkondo mpana zaidi katika kipindi cha uongozi wa Rais Donald Trump. Katika fremu hiyo, Washington ikiwa na lengo la kuwafanya Wapalestina wasalimu amri mbele ya uchu na tamaa za Marekani na Israel imeamua kuwashinikkiza zaidi kifedha Wapalestina.

Maandamano ya kuunga mkono UNRWA

Kwa hakika hatua hizo zimedhihirisha wazi kwamba, madai ya Marekani ya kutoa misaada ya kibinadamu bila malengo mengine yoyote ni urongo na hadaa tupu. Fauka ya hayo, kushtadi siasa za Marekani katika kuzishiniklia jumuiya za kimataifa ili zifuate matakwa yake, kwa namna fulani kunahesabiwa kuwa ni kuomba rushwa. Hatua hizo za Marekani zimekabiliwa na ukosoaji mkubwa wa asasi na jumuiya hizo na bila shaka migomo na malalamiko ya wafanyakazi wa asasi hizo dhidi ya utendaji huo wa Marekani ni mambo ambayo yanapaswa kutathminiwa katika uwanja huo.

Sami Abu Zuhri, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameitathmini hatua hiyo ya Marekani ya kusitisha misaada yake kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA kuwa ni mpango hatari wa nchi hiyo dhidi ya haki za taifa la Palestina.  Abu Zuhri anasema:

Hatua ya hivi karibuni ya Marekani kupunguza na kutishia kusimamisha kikamilifu misaada yake ya kifedha kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA kunafanyika kwa ajili ya kufutilia mbali haki ya wakimbizi wa Kipalestina ya kurejea makwao.

Sami Abu Zuhri, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa Hamas

Kwa hakika kupunguzwa na baadaye kukatwa kabisa misaada ya Marekani kwa shirika la UNRWA kivitendo kunalenga kusitisha shughuli za asasi amilifu za misaada ya kibinadamu katika mgogoro wa Palestina na hivyo kuandaa uwanja na mazingira ya kuifuta kabisa kadhia ya Palestina.

Hata hivyo radiamali za asasi mbalimbali za Umoja wa Mataifa kwa hatua za Marekani katika miezi ya hivi karibuni dhidi ya Wapalestina ukiwemo upinzani wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa uamuzi wa Trump kuhusu Beitul-Muqaddas ulikuwa sawa na mshtuko wa kidiplomasia wa Umoja wa Mataifa kwa utawala vamizi wa Israel na waungaji mkono wake hususan Marekani.

Bila shaka matukio haya yameonyesha kwamba, harakati yoyote ile ya Marekani ya kufuata siasa za kivamizi za Israel huko Quds zinaweza kuwa na gharama kubwa ya kisiasa na kidipolmasia kwa Washington.