Marekani inajiandaa kuishambulia Syria kwa makombora
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i40253-marekani_inajiandaa_kuishambulia_syria_kwa_makombora
Chombo kimoja cha habari nchini Marekani kimeripoti kuwa Washington inajiandaa kuishambulia Syria kwa makombora.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2018 01:11 UTC
  • Marekani inajiandaa kuishambulia Syria kwa makombora

Chombo kimoja cha habari nchini Marekani kimeripoti kuwa Washington inajiandaa kuishambulia Syria kwa makombora.

Shirika la habari la Associated Press limetangaza kuwa Marekani inakusudia kuvishambulia kwa makombora ya Tomahawk baadhi ya vituo muhimu vya kijeshi nchini Syria.

Katika muda wa mwezi mmoja uliopita, viongozi wa Marekani wamekuwa wakieneza tuhuma bandia dhidi ya jeshi la Syria kwamba eti limetumia gesi za sumu, madai ambayo yamekadhibishwa vikali na viongozi wa nchi hiyo.

Kuhusiana na suala hilo, Marekani imewasilisha ripoti kadhaa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa ni katika juhudi za kuandaa mazingira ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya serikali ya Damascus lakini imekuwa ikikabiliwa na upinzani wa Russia.

Makamanda wa jeshi la Russia wameeleza wasiwasi walionao kutokana na uenezaji wa ripoti hizo na kutangaza kwamba endapo Marekani itavishambulia vituo vya jeshi la Syria, uhusiano wa Moscow na Washington utakuwa wa mivutano zaidi kuliko ulivyo hivi sasa.

Askari wa jeshi la Syria na wapiganaji wa kujitolea baada ya ushindi katika medani za vita dhidi ya magaidi

Itakumbukwa kuwa mwezi Aprili mwaka uliopita wa 2017, jeshi la Marekani lilikishambulia kwa makombora 59 ya Tomahawk kituo cha anga cha jeshi la Syria cha Shayrat.

Katika kuhalalisha hujuma yake hiyo, jeshi la Marekani lilidai kwamba hujuma hiyo ilikuwa jibu kwa shambulio la silaha za kemikali lililofanywa na jeshi la Syria katika eneo la Khan Shaikhun mkoani Idlib magharibi mwa nchi hiyo.

Wataalamu wengi wanaitakidi kuwa kuituhumu serikali ya Syria kuwa imetumia silaha za kemikali ni kujaribu kuzipotosha fikra za waliowengi na kuipindua ukweli halisi ili kukabiliana na ushindi liliopata hivi karibuni jeshi la Syria na mhimili wa muqawama dhidi ya magaidi wanaoungwa mkono na baadhi ya madola ya Magharibi na waitifaki wao katika eneo la Mashariki ya Kati.../