Wakristo Quds: Tutaendelea kuwashinda Wazayuni waliozivamia ardhi za Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i41003-wakristo_quds_tutaendelea_kuwashinda_wazayuni_waliozivamia_ardhi_za_palestina
Wakristo wa mji wa Quds wamefurahishwa na hatua ya kufunguliwa upya kanisa kuu la 'Al-Qiyamah' baada ya kufungwa kwa siku kadhaa na utawala haramu wa Israel na kuitaja hatua hiyo kuwa ni katika safari ya kuelekea ushindi kamili dhidi ya Wazayuni hao wanaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 01, 2018 04:38 UTC
  • Wakristo Quds: Tutaendelea kuwashinda Wazayuni waliozivamia ardhi za Palestina

Wakristo wa mji wa Quds wamefurahishwa na hatua ya kufunguliwa upya kanisa kuu la 'Al-Qiyamah' baada ya kufungwa kwa siku kadhaa na utawala haramu wa Israel na kuitaja hatua hiyo kuwa ni katika safari ya kuelekea ushindi kamili dhidi ya Wazayuni hao wanaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni baada ya kufunguliwa milango ya kanisa hilo jana asubuhi baada ya kufungwa kwa siku tatu na Wazayuni ikiwa ni katika kutekeleza hatua za kuyalazimisha makanisa ya mji wa Quds kulipa kodi kwa utawala bandia wa Israel.

Moja ya makanisa katika mji wa Quds, Palestina ambayo Israel inakusudia kuyafunga

Kufuatia hali hiyo viongozi wa Kikristo mjini Quds (Jerusalem) wakizungumzia hatua ya kufunguliwa kanisa hilo la Al-Qiyamah wameshukuru juhudi za shakhsia na asasi mbalimbali zilizofanikisha suala hilo huku wakizitaka asasi hizo kuendeleza juhudi hizo kwa ajili ya kulinda uwepo wao katika mji huo. Kadhalika Wakristo wa mji wa Quds wametoa mwito kwa asasi hizo kutetea mji huo kutokana na njama chafu za utawala haramu wa Kizayuni. Wakiashiria vitisho na hatari inayowakabili Wakristo na Waislamu wanaoishi mji huo ambao unaenziwa na wafuasi wa dini tatu za mbinguni, wamesema kuwa jana makanisa yalishinda vita na utawala wa Kizayuni ambao ulitaka kuyafunga makanisa hayo. Baada ya mashinikizo mbalimbali hatimaye Israel ililazimika kusimamisha zoezi la kuyatoza kodi makanisa ya mji huo huku ikiahidi kuendeleza zoezi hilo hapo baadaye.

Viongozi wa Kikristo mjini Quds wakilalamikia njama chafu za Mazayuni 

Wakati huo huo, Nabil Abou Dordaneh Msemaji wa ikulu ya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameitaja hatua ya usitishaji tu zoezi hilo kuwa isiyotosha na ameitaka Tel Aviv kukoma kuchezea matukufu ya Waislamu na Wakristo katika mji wa Quds na maeneo mengine ya Palestina. Inafaa kuashiria kwamba, Waislamu na Wakristo katika ardhi za Palestina wanapitia wakati mgumu ambapo Israel imekuwa ikiwakandamiza na kuwadhalilisha kwa lengo la kuwaondoa katika mji huo kupitia mpango wa kuuyahudisha kikamilifu mji wa Quds (Jerusalem).