Rais Assad aahidi kuvunja njama za Wamagharibi dhidi ya Syria
Rais wa Syria, Bashar al-Assad ameahidi kupambana kikamilifu na njama za Wamagharibi zinazolenga kuvunja umoja wa wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Katika ujumbe uliochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa Ofisi ya Rais wa Syria katika mtandao wa kijamii wa Telegram, Rais Assad amesema vita dhidi ya ugaidi nchini humo havitakoma madhali kuna gaidi mmoja aliyesalia katika ardhi ya nchi hiyo.
Amesema, "Tutaendelea kukabiliana na senario zote za Wamagharibi wanaotaka kuhujumu umoja wa wananchi na uhuru wa kujitawala nchi hii."
Rais wa Syria ametahadharisha kuwa, lengo la nchi za Magharibi ni kuhakikisha kuwa wanaigawanya Syria mapande mapande.
Mapema mwezi huu, Rais wa Syria alisema muungano wa kimataifa unaodaiwa kuwa 'dhidi ya Daesh' chini ya uongozi wa Marekani, kwa sasa umegeuka na kuwa kikosi cha anga cha kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Syria.
Serikali ya Damascus imekuwa ikisisitiza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel na nchi za Magharibi na waitifaki wao katika eneo wanayaunga mkono kwa hali na mali magenge ya kigaidi yanayovuruga usalama na uthabiti nchini Syria tangu Machi mwaka 2011.