Assad: Kila mara Muqawama unapopata ushindi Wamagharibi wanapiga makelele
(last modified Thu, 12 Apr 2018 14:49:56 GMT )
Apr 12, 2018 14:49 UTC
  • Assad: Kila mara Muqawama unapopata ushindi Wamagharibi wanapiga makelele

Rais Bashar Assad wa Syria amesema kuwa nchi za Magharibi zimekuwa zikizusha makelele kila mara muqawama na mapambano dhidi ya magaidi na washirika wao yanapopata ushindi na mafanikio.

Rais Bashar Assad wa Syria ameyasema hayo leo katika mazungumzo yake na Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika Masuala ya Kimataifa aliyeko safarini mjini Damascus. 

Rais wa Syria ameashiria vitisho vya Marekani vya kutaka kuishambulia Syria na kusema: Harakati yoyote ya Wamagharibi dhidi ya Syria itachafua zaidi usalama wa Mashariki ya Kati na kuhatarisha amani na usalama wa kimataifa. Amesisitiza kuwa, harakati zinazotia wasiwasi za hivi karibuni za Wamagharibi zinafanyika kwa shabaha ya kuvuruga mlingano wa nguvu katika medani ya vita kwa maslahi ya makundi ya kigaidi.

Bashar Assad amesema kuwa, baada ya kukombolewa eneo la Ghouta Mashariki, Wamagharibi wamekuwa wakizungumzia suala la kuishambulia Syria kwa kutegemea urongo wa kutumiwa silaha za kemikali katika eneo hilo na suala hili linaonesha kuwa, wamefeli katika mahesabu yao katika vita vya Syria.

Jeshi la Syria limekomboa eneo la Ghouta Mashariki

Kwa upande wake Mshauri wa Kiongozi Mkuu wa Iran katika Masuala ya Kimataifa Ali Akbar Velayati amesema kuwa, vita vya pande zote dhidi ya taifa na serikali ya Syria vilianzishwa miaka saba iliyopita vikizishirikisha makumi ya nchi chini ya uongozi wa moja kwa moja wa Marekani. Velayati ameongeza kuwa, Syria haijadhoofika kuliko ilivyokuwa miaka saba iliyopita wala Marekani haijapata nguvu zaidi. 

Maafisa wa Marekani akiwemo Rais Donald Trump na Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo James Mattis wamekuwa wakipiga ngoma za vita na mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria kwa kisingizio cha kutumiwa silaha za sumu ya kemikali katika eneo la Ghouta Mashariki. Serikali ya Damascus imekadhibisha vikali madai hayo.