Kimbunga kikali chaua watu 3 Oman, zaidi ya 7 Yemen
Watu watatu wamepoteza maisha nchini Oman kufuatia kimbunga kikali ambacho kinaendelea kukumba pwani ya kusini mwa nchi hiyo eneo la Salalah.
Wakuu wa Oman wanasema miongoni mwa waliopoteza maisha ni msichana ya miaka 12 huku idadi kubwa ya watu nao wakiripotiwa kutoweka.
Kimbunga hicho ambacho ambacho kimepewa jina la Mekunu kimesababisha maafa hasa katika mikoa ya Dhofar na al Wusta nchini Oman. Taarifa zinasema kimbunga hicho kimesababisha hasara kubwa katika Kisiwa cha Socootra nchini Yemen ambapo watu saba wanaripotiwa kupoteza maisha . Aidha maeneo ya kaskazini magharibi mwa Saudi Arabia pia yamekumbwa na kimbunga hicho na hadi sasa hakuna taarifa za maafa au hasara.
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Oman imetahadharisha kuwa mikoa ya Dhofar na al Wusta itaendelea kushuhudia mvua na upepo mkali huku bahari ikichafuka na mawimbi yakitazamiwa kufika mita nane. Idara ya Usafiri wa Anga Oman Jumamosi hii imefungua tena Uwanja wa Ndege wa Salalah ambao ulikuwa umefungwa kwa muda wa siku tatu. Hata hivyo shule katika eneo hilo zitaendelea kufungwa hadi Jumatatu.