Rais Assad: Wanajeshi wa Marekani lazima tutawatimua Syria
Rais Bashar al Assad wa Syria amesema kuwa, Wamarekani lazima watoke Syria na wanapaswa kupata funzo kutokana na yaliyowafika nchini Iraq
Rais Assad amesisitiza hayo wakati alipohojiwa na televisheni ya Russia Today na kuongeza kuwa: Licha ya kwamba jeshi la Syria linazidi kupata ushindi katika vita vyake vya kupambana na magaidi, lakini kila ushindi linaoupata jeshi hilo unaifanya Marekani, Israel na baadhi ya nchi za Magharibi kufanya njama za kuchelewesha kupatikana ushindi kamili kupitia kuwaunga mkono waziwazi magaidi na kuzidi kuwamimina magaidi hao kutoka nje ya Syria au kukwamisha juhudi za kisiasa za kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa nchi hiyo.

Rais wa Syria aidha amesema, baada ya kukombolewa Halab, Deir ez-Zor, Homs na Damascus, Marekani na Israel zimepoteza sehemu kubwa ya uchochezi wao ambao zilikuwa zikiufanya kupitia magenge ya kigaidi kama Daesh na Jabhat al Nusra na hivi sasa wamebakiwa na chaguo moja tu la kutumia makundi kama lile linaloitwa Vikosi vya Demokrasia vya Syria.
Rais Assad amesisitiza pia kuwa, maeneo yote yaliyoko mikononi mwa kundi hilo nayo yatakombolewa bila ya wasiwasi wowote. Ameongeza kuwa, kuna machaguo mawili ya kuamiliana na kundi hilo linayojiita vikosi vya demokrasia, chaguo la kwanza ni kupitia mazungumzo na la pili ni kutumia nguvu za kijeshi. Amesema, kipaumbele cha juu kabisa ni hilo chaguo la kwanza la mazungumzo, na kama mazungumzo yatashindwa kulilazimisha kundi hilo kutoka katika maeneo linayoyakalia kwa mabavu, basi kutatumika nguvu za kijeshi kuyakomboa.
Vile vile amekanusha madai ya Israel kuwa eti Iran imetuma jeshi nchini Syria na kuongeza kuwa, ilichofanya Iran ni kuitikia ombi la serikali ya Syria la kutuma washauri wa kijeshi nchini humo. Vile vile amesema, Syria itaendelea kukabiliana na mashambulizi ya anga ya Israel kwa nguvu zake zote.