Marekani kupanua operesheni zake za kijeshi Yemen kufuatia ombi la Imarati
Marekani inatathmini ombi la Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) la kuipa msaada wa moja kwa moja kwa ajili ya kufanikisha mashambulizi ya kuiteka bandari ya Hudaydah, ambayo kwa sasa inadhibitiwa na vikosi vya Ansarullah vya Yemen.
Maofisa wa Marekani wamesema tayari Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ametoa agizo la kutathminiwa ombi hilo la Imarati la kupewa uungwaji mkono wa moja kwa moja na Washington, ikiwemo kuipa ndege za kijeshi zisizo na rubani.
Ingawa Marekani, Uingereza, utawala wa Kizayuni wa Israel zimekuwa zikishiriki moja kwa moja kwenye vita dhidi ya wananchi wa Yemen, lakini afisa mmoja wa ngazi za juu wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe amenukuliwa na jarida la The Wall Street Journal akisema kuwa, "Saudi Arabia na Imarati zimekiri kuwa haziwezikuitwaa bandari hiyo ya kistratajia iliyoko katika Bahari Nyekundu bila ya baraka na msaada zaidi wa Marekani."
Hata hivyo ofisa mwingine wa Marekani ameonyesha wasi wasi mkubwa juu ya ombi hilo, akisema kuwa, hawana uhakika wa 100% kuhusu mashambulizi ya muungano wa kijeshi wa Saudia
Ieleweke kuwa, bandari ya al-Hudaydah ndio njia muhimu kwa taifa la Yemen ambapo karibu asilimia 80 ya misaada ya kibinaadamu ikiwemo chakula na madawa kwa ajili ya raia wa nchi hiyo hupitia katika bandari hiyo.
Mara kadhaa Umoja wa Mataifa umeutaka muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia kutofanya shambulizi lolote dhidi ya mji wa bandari hiyo ambao ni nukta pekee iliyosalia kwa ajili ya kuingiza misaada ya kibinaadamu kwa ajili ya wananchi wa Yemen.