OPCW: Hakuna ushahidi wa kutekelezwa shambulizi la kemikali Douma, Syria
Uchunguzi wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) umebainisha kwamba hakuna shambulizi lolote la silaha za kemikali lililofanyika katika mji wa Douma, ulioko katika viunga ya mji mkuu wa Syria, Damascus.
Ripoti ya uchunguzi huo iliyotolewa jana Ijumaa imesema kuwa, sampuli mbili za mitungi ya gesi iliyopatikana katika maeneo kulikodaiwa kufanyika mashambulizi hayo zilikuwa na chembechembe za kemikali nyepesi ya Chlorine ambayo hutumika sana katika maeneo hayo, na wala sio kemikali hatari za sumu kama ilivyodaiwa hapo awali.
Wakaguzi wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) walielekea Syria kwa ajili ya kuchunguza maeneo kunakodaiwa kwamba kulitumiwa silaha za kemikali tarehe 7 Aprili, wiki moja baada ya kuibuliwa madai hayo.
Madai hayo yalitumiwa na nchi za Marekani, Uingereza na Ufaransa kama kisingizio cha kushambulia maeneo kadhaa na vituo vya utafiti ndani ya nchi ya Syria kabla hata ya kufanyika uchunguzi wa aina yoyote kuhusu madai hayo.
Mashambulizi hayo pia yalifanyika bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Russia na Syria zilipuuzilia mbali madai hayo ya kufanyika hujuma za kemikali hatari ya sumu aina ya Organophosphorus mjini Douma.