Palestina yateuliwa kuongoza Kundi la 77 la UN
Palestina imeteuliwa kuwa mwenyekiti wa kiduru wa Kundi la 77 (G77) linalojihusisha na masuala ya uchumi wa nchi zinazostawi, ambazo zinaunda asilimia 80 ya idadi ya watu wote duniani.
Hatua hiyo ya kuteuliwa Palestina kuchukua uenyekiti wa kundi hilo kubwa zaidi katika Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala la maendeleo katika nchi za ulimwengu wa tatu imeutia kiwewe utawala haramu wa Israel.
Riyad Mansour, Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema Palestina itaanza rasmi kuwa mwenyekiti wa Kundi la 77 kuanzia Januari mwakani , kuchukua nafasi inayoshikiliwa kwa sasa na Misri ya kuziwakilisha nchi 135 katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
G77 ilianziswa mwaka 1964 na nchi 77 zinazostawi na sasa kundi hilo limepanuka na lina wanachama 135.
Hivi karibuni, Palestina iliruhusiwa kujiunga na Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) na Wakala wa Maendeleo ya Viwanda wa Umoja wa Mataifa (UNIDO), pamoja na Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OCPW), hatua ambayo ilizitia kiwewe pia Marekani na utawala pandikizi wa Israel.
Aidha Oktoba mwaka jana, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zilitangaza kujiondoa katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), baada ya Palestina kuruhusiwa kujiunga na shirika hilo.
Aidha Tel Aviv na Washington zilighadhabishwa mno na kitendo cha Palestina kuruhusiwa kujiunga na Mkataba wa Roma uliounda Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC Januari mwaka 2015.