Amnesty International: Imarati inahusika na jinai zinazojiri Yemen
Shirika la Msamaha Duniani Amnesty International limetangaza kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) inahusika na kuteswa na kupotea watu katika maeneo mbalimbali huko Yemen.
Shirika hilo limetangaza kuwa wanajeshi wa Imarati na nchi nyingine katika muungano vamizi wa Saudi Arabia wanahusika katika matukio mbalimbali kama ya kuteswa na kupotea watu katika maeneo mbalimbali ambayo yanashikiliwa na vikosi hivyo huko Yemen.
Saudia ikiungwa mkono na Imarati, Marekani na nchi kadhaa mwezi Machi 2015 ilianzisha hujuma ya kijeshi dhidi ya Yemen na kisha kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, nchi kavu na anga. Mashambulizi hayo ya Saudia na wiatifaki wake huko Yemen hadi sasa yamesababisha vifo vya Wayamani zaidi ya elfu 17, kujeruhi makumi ya maelfu na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya wengine. Uvamizi huo wa kijeshi wa Saudia huko Yemen umeifanya nchi hiyo maskini kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na dawa. Taasisi za kimataifa na zile za haki za binadamu zimezitaka Marekani, Uingereza na nchi nyingine zinazouunga mkono utawala wa Saudia kuacha kuiuzia silaha Riyadh.
Wakati huo huo Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limetangaza kuwa Marekani na Uingereza zimeiuzia Saudi Arabia silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola na kuongeza kuwa utawala wa Saudia umetumia silaha hizo kuua wanafunzi wa Yemen katika mji wa Dhayhan katika mkoa wa Saada.