Hizbullah: Marekani haina ubavu wa kuwawekea masharti walioshinda vita Syria
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imesema kuwa Marekani ambayo sera zake za kuyasaidia makundi ya kigaidi kwa ajili ya kuindoa madarakani serikali halali ya Syria zimefeli na kushindwa haina haki na ubavu wa kutoa masharti ya kuondoka washauri wa kijeshi wa Iran na wapiganaji wa Hizbullah nchini Syria ambao wameshinda vita dhidi ya magaidi.
Naibu katibu Mkuu wa Hizbullah, Sheikh Naim Qassem amesema masharti yaliyotolewa na Marekani kwa serikali ya Syria hayana maana yoyote na kuongeza kuwa walioshinda vita dhidi ya ugaidi ndio wenye haki na uwezo wa kutoa masharti na si Marekani iliyoshindwa huko Syria.
Sheikh Naim Qassem amepongeza mafanikio ya jeshi la Syria na waitifaki wake ambao wameweza kuyashinda makundi ya kigaidi yanayosaidiwa na kuungwa mkono na Marekani, Israel, Saudi Arabia na washirika wao.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah pia ameyataka makundi yote yanayoitegemea Marekani kutazama upya uhusiano wao na "Shetani Mkubwa" kwa sababu kamwe si mwaminifu kwa marafiki zake.
Matamshi hayo yametolewa baada ya vyombo vya habari kufichua kuwa, ujumbe wa Marekani uliojumuisha maafisa wa usalama na vyombo vya ujasusi umezuru Damascus na kukutana na mshauri maalumu wa usalama wa Rais wa nchi hiyo, Ali Mamlouk.
Inasemekana kuwa katika mazungumzo ya pande hizo mbili Marekani ilitoa masharti kadhaa ya kuondoa wanajeshi wake katika ardhi ya Syria ikiwa ni pamoja na kuondoka washauri wa masuala ya kijeshi wa Iran huko kusini mwa Syria karibu na eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel la Golan na kupewa nafasi katika miradi ya biashara ya mafuta huko mashariki mwa Syria.