Ripoti: Njaa yawalazimisha Wayemen kula majani
Inaarifiwa kuwa, wananchi wa Yemen wanalazimika kula majani ya miti kutokana na kusakamwa na baa la njaa sambamba na kukosa kitu cha kula, huku mgogoro wa kibinadamu katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu ukiingia katika hatua ya kuogofya.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, wakazi wa wilaya ya Aslam katika mkoa wa Hajjah, kaskazini magharibi mwa Yemen wanategemea majani ya miti ili kupunguza makali ya njaa inayowasakama.
Habari zinasema kuwa, akina mama katika maeneo hayo huchuma majani ya mti aina ya Halas au Wax kwa Kiingereza, na kuyaosha kabla ya kuyachemsha na kuyala.
Hii ni licha ya majani hayo kuwa machachu na yenye asidi kali yakishachemshwa.

Hii ni katika hali ambayo, Mpango wa Chakula Duniani wa Umoja wa Mataifa (WFP) umetahadharisha katika taarifa yake juu ya mwenendo wa kuwafikishia misaada wananchi wa Yemen wanaokabiliwa na baa la njaa ambalo limesababishwa na mashambulio ya kijeshi na mzingiro wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia na kutoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kukabiliana na hali hiyo.
Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani, Israel, Imarati na nchi nyingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen mwezi Machi mwaka 2015, na hadi sasa maelfu ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.