Wikileaks: Saudia imeyahonga magazeti ya UK ili yasiripoti mauaji ya Khashoggi
Mtandao wa WikiLeaks umefichua kuwa, magazeti ya Uingereza hayajaakisi habari za mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia aliyeuliwa katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki, kwa kuwa yamemwagiwa pesa na utawala wa Riyadh.
Mtandao wa Wikileaks ambao ni maarufu kwa kufichua kashfa za ufisadi wa kifedha umebainisha kuwa, magazeti na mashirika yote ya habari duniani yakiwemo Reuters na Associated Press yameripoti kuhusu muaji hayo, lakini magazeti ya Uingereza yameifumbia macho habari hiyo kwa kuwa yamepokea pesa nyingi za Saudia.
Wikileaks imeeleza kushangazwa kwake na magazeti ya Uingereza ambayo hivi karibuni yalichangamkia habari kuhusu kile kilichodaiwa kuwa ni mauaji ya mwandishi wa habari wa Russia, Arkady Babchenko, ambaye mwishowe iligundulika kuwa hajauawa, lakini yamepuuza kabisa kuakisi habari ya kutoweka kwa Jamal Khashoggi katika mazingira ya kutatanisha.
Televisheni ya Aljazeera ya Qatar imetangaza kuwa maiti ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari mkosoaji wa utawala wa Saudia imeokotwa kwenye eneo moja la mji wa Istanbul, Uturuki.
Jina la Khashoggi lilikuwemo kwenye orodha ya watu wanaofuatiliwa kutiwa nguvuni na utawala wa Aal Saud, hivyo kutokana na kuhofia kukamatwa, alikuwa akiishi nje ya Saudi Arabia.