Mashambulizi mapya ya anga ya US yaua makumi ya raia Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i48919-mashambulizi_mapya_ya_anga_ya_us_yaua_makumi_ya_raia_syria
Kwa akali raia 32 wameuawa katika hujuma mpya ya anga iliyofanywa na ndege za kivita za muungano wa kijeshi unaongozwa na Marekani katika mkoa wa Dayr al-Zawr, mashariki mwa Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 20, 2018 04:32 UTC
  • Mashambulizi mapya ya anga ya US yaua makumi ya raia Syria

Kwa akali raia 32 wameuawa katika hujuma mpya ya anga iliyofanywa na ndege za kivita za muungano wa kijeshi unaongozwa na Marekani katika mkoa wa Dayr al-Zawr, mashariki mwa Syria.

Shirika la Syrian Observatory for Human Rights (SOHR) limesema raia 18 wakiwemo watoto saba wameuawa katika mashambulizi hayo mapya ya Marekani katika mkoa huo wenye utajiri wa mafuta nchini Syria siku ya Alkhamisi, huku 14 wakiuawa hapo jana Ijumaa.

Taarifa ya shirika hilo eti la kutetea haki za binadamu imeongeza kuwa, wanachama tisa wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh pia wameuawa katika mashambulizi hayo ya anga ya Marekani. 

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Walid al Mualim alisema Marekani haifuatilii malengo yake pekee nchini Syria bali pia inatekeleza sera za Israel nchini humo.

Ndege za kivita za Marekani zinazodai kupambana na magaidi Syria

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa hujuma kubwa ya makundi ya kigaidi yakisaidiwa kwa hali na mali na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao, lengo likiwa ni kubadili mlingano wa nguvu katika eneo la Mashariki ya Kati kwa maslahi ya utawala haramu wa Israeli. 

Hata hivyo kusimama kidete jeshi la Syria na waitifaki wake mbele ya njama dhidi ya taifa hilo  kumesambaratisha njama za maadui hao na kuvuruga mahesabu yao yote.