Jeshi la Israel laendeleza ukatili wake, laua Wapalestina 5 Ghaza
(last modified Sat, 27 Oct 2018 05:52:39 GMT )
Oct 27, 2018 05:52 UTC
  • Jeshi la Israel laendeleza ukatili wake, laua Wapalestina 5 Ghaza

Kwa akali Wapalestina watano wameuawa shahidi huku mamia ya wengine wakijeruhiwa baada ya jeshi la Israel kuwamiminia risasi na kuvurumishia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji wa Kipalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Wizara ya Afya ya Ghaza imesema waliouawa katika maandamano ya jana Ijumaa katika Ukanda wa Ghaza ni vijana mabarobaro waliokuwa na umri wa kati ya miaka 19 na 27. 

Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, makumi ya watoto na wanawake ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa kwa silaha za jeshi katili la Israel katika maandamano hayo ya amani. 

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel bila kuzungumzia chochote kuhusu waliouawa au kujeruhiwa, limesema lililazimika kutumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano hayo ya watu zaidi ya 10,000.

Maandamano ya amani yaliyopewa jina la "Haki ya Kurejea" yalianza tarehe 30 Machi mwaka huu kwa mnasaba wa Siku ya Ardhi huko Ukanda wa Ghaza na yangali yanaendelea.

Maandamano ya Haki ya Kurejea Ghaza

Tangu wakati huo hadi sasa zaidi ya Wapalestina 212 wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Israel na wengine 17,500 wamejeruhiwa.

Maandamano hayo yamewatia kiwewe viongozi wa utawala dhalimu wa Israel na ndio maana wamekuwa wakiwafyatulia risasi na mambomu ya kutoa machozi waandamanaji na kuwaua ovyo.