Ndege za kivita za Marekani zaua raia wengine 15 Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49263-ndege_za_kivita_za_marekani_zaua_raia_wengine_15_syria
Kwa mara nyingine tena ndege za muungano wa kijeshi wa Marekani zimetekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya wakazi wa mkoa wa Dayr al-Zawr, mashariki mwa Syria na kuua raia 15.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 04, 2018 04:22 UTC
  • Ndege za kivita za Marekani zaua raia wengine 15 Syria

Kwa mara nyingine tena ndege za muungano wa kijeshi wa Marekani zimetekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya wakazi wa mkoa wa Dayr al-Zawr, mashariki mwa Syria na kuua raia 15.

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limeripoti kuwa, aghalabu ya waliouawa katika hujuma hiyo ya jana katika eneo la Hajin ni wanawake na watoto wadogo na kwamba idadi kubwa ya raia wasio na ulinzi wamejeruhiwa kwenye mashambulizi hayo ya anga.

Haya yanajiri chini ya mwezi mmoja baada ya Bashar al-Ja'afari, Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa kulithibitishia Baraza la Usalama la umoja huo kuwa muungano huo vamizi unaoongozwa na Marekani umetumia mabomu hatari ya fosforasi nyeupe dhidi ya eneo hilo hilo la Hajin, yapata kilomita 110 mashariki mwa mkoa wa Dayr al-Zawr.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, serikali ya Syria iliuandikia barua Umoja wa Mataifa ikiutaka ufanye uchunguzi wa wazi na usiogemea upande wowote juu ya mashambulizi ya anga ya hivi karibuni ya muungano wa kijeshi wa Marekani dhidi ya wakazi wa mkoa huo wa Dayr al-Zawr, mashariki mwa nchi hiyo ya Kiarabu. Barua hiyo iliyataja mashambulizi hayo kama mauaji ya halaiki, jinai ya kivita na jinai dhidi ya binadamu. 

Mji wa Hajin mkoani Dayr al-Zawr

Mashambulizi hayo mapya ya Marekani katika vijiji vya al-Sousa and al-Bubadran vilivyoko katika mkoa huo wenye utajiri wa mafuta, mashariki mwa Syria mwezi uliopita yalipelekea kuuawa raia 62, akthari yao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo. 

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa hujuma kubwa ya makundi ya kigaidi yakisaidiwa kwa hali na mali na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao, lengo likiwa ni kubadili mlingano wa nguvu katika eneo la Mashariki ya Kati kwa maslahi ya utawala haramu wa Israeli.