Oxfam: Sera za Uingereza juu ya Yemen ni za kukinzana
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49264-oxfam_sera_za_uingereza_juu_ya_yemen_ni_za_kukinzana
Shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam limekosoa vikali hatua ya Uingereza ya kukataa kusimamisha uuzaji wa silaha zake kwa Saudi Arabia, ambazo mbali na kusababisha mauaji ya raia wa nchi maskini ya Yemen, pia zinatumika kuharibu misaada ya kibinadamu ya shirika hilo kwa Wayemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 04, 2018 04:28 UTC
  • Oxfam: Sera za Uingereza juu ya Yemen ni za kukinzana

Shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam limekosoa vikali hatua ya Uingereza ya kukataa kusimamisha uuzaji wa silaha zake kwa Saudi Arabia, ambazo mbali na kusababisha mauaji ya raia wa nchi maskini ya Yemen, pia zinatumika kuharibu misaada ya kibinadamu ya shirika hilo kwa Wayemen.

Dina el-Mamoun, afisa wa Oxfam ameiambia Kamati ya Kimataifa ya Maendeleo ya Bunge la Uingereza kuwa, ni kinaya kuwa silaha za Uingereza zinatumika kuharibu shehena za misaada ya kibinadamu iliyotoka na serikali ya London kwa wananchi wa Yemen.

Toni Pearce, afisa mwengine wa shirika hilo la misaada ya kibinadamu la Uingereza ameiambia kamati hiyo kuwa, "Kwa upande mmoja, Uingereza inatoa misaada ya dharura kwa wananchi wa Yemen, na kwa upande wa pili inaendelea kuizuia Saudia silaha zinazotumika kuharibu misaada hiyo na kupelekea kupotea maisha ya idadi kubwa ya Wayemen hao kutokana na mapigano, magonjwa na njaa."

Oxfam imesisitiza kuwa, Uingereza  ina nafasi nzuri sana ya kugeuza mkondo wa vita nchini Yemen, kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Makombora ya Saudia iliyouziwa na Ulaya yakivurumishwa Yemen

Huko nyuma pia, shirika hilo la misaada ya kibinadamu lililaani jinai zinazoendelea kufanywa na muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia dhidi ya wananchi wa Yemen ikiwa ni pamoja na kuzuia kufikiwa na chakula, mafuta na madawa Wayemen licha ya wananchi hao kuwa na majanga yasiyoelezeka.

Ikumbukwe kuwa Marekani na nchi za Magharibi hasa Uingereza ndio wauzaji wakuu wa silaha zinazotumiwa na Saudi Arabia na wapambe wake kufanya jinai za kinyama nchini Yemen, ambapo hadi hivi sasa zaidi ya watu 15 elfu wameshauawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa.