Ufaransa yataka kusimamishwa vita vya Saudia dhidi ya Yemen
-
Jean-Yves Le Drian
Katika hatua iliyochukuliwa kwa kuchelewa ya nchi za Magharibi kuhusu mauaji yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia huko Yemen, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ameitaka jamii ya kimataifa kukomesha vita na mashambulizi ya Saudia dhidi ya watu wa Yemen.
Jean-Yves Le Drian ambaye ameyataja mashambulizi ya Saudia huko Yemen kuwa ni "vita chafu", amekiri kuwa vita hiyo haina mshindi na kwamba kuna udharura wa kukomeshwa na kuepusha ufujaji wa gharama zake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ameashiria kikao kijacho kuhusu Yemen kilichopangwa kufanyika barani Ulaya na amezitaka pande zote kufanya jitihada za kusitisha vita, kusaidia operesheni za kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wathirika na kudumisha mazungumzo ya kisiasa.
Ikumbukwe kuwa katika kipindi chote cha vita na mashambulizi ya miezi 44 sasa ya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen, Ufaransa ilikuwa miongoni mwa wadhamini wakuu wa silaha na zana za kivita kwa utawala wa Riyadh.
Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alikuwa amesema kuwa jamii ya kimataifa imeafikiana kwamba, vita dhidi ya Yemen inapaswa kusitishwa.
Maelfu ya raia wasio na hatia wa Yemen wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya Saudia na washirika wake yaliyoanza mwezi Machi mwaka 2015.