Hizbullah ya Iraq: Muqawama utakata mikono itakayoichokoza Iran
Msemaji wa brigedi za harakati ya Hizbullah ya Iraq amejibu matamshi ya karibuni ya Rais wa Marekani kwa kusema kuwa: Trump asahau njonzi ya kutaka kuishambulia kijeshi Iran kutokea Iraq kwa sababu muqawama wa Iraq utakata mikono ya mchokozi wa aina hiyo.
Akizungumza juzi Jumapili katika mahojiano na televisheni ya CBS News ya nchini Marekani, Rais Donald Trump alidai kuwa wanajeshi wa nchi yake wanaendelea kuwepo huko Iraq ili kuweza kuifuatilia kwa karibu Iran. Jaafar al Husseini msemaji wa brigedi za harakati ya Hizbullah ya Iraq jana Jumatatu alisisitiza kuwa wabunge wa Iraq wanapasa kuandaa rasimu ya sheria kwa ajili ya kuondoka nchini humo wanajeshi wa Marekani. Aidha aliongeza kuwa, jukumu jipya la jeshi la Marekani kwa mujibu wa matamshi yaliyobainishwa na Trump limeeleweka wazi, na kwamba makundi ya muqawama ya Iraq yako macho mbele ya nia mbaya na ya uhasama ya Marekani.
Msemaji wa brigedi za harakati ya Hizbullah ya Iraq ameyataja matamshi hayo ya Trump katika mahojiano ya televisheni ya CBS News kuwa ni kinyume na msimamo rasmi wa Iraq na yanapuuza mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo. Amesema wanajeshi wa Marekani hawaruhusiwi kuendesha harakati zao katika maeneo ya mipaka na kufanya mashambulizi kwenye maeneo hayo.