Imarati yashutumiwa kufanya njama za kurejesha utawala wa kidikteta Tunisia
Waziri Mkuu wa zamani wa Tunisia amefichua kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) unafanya njama za kufelisha juhudi za kuimarisha demokrasia nchini humo kupitia hilo za kuyafelisha mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo na kuurejesha madarakani utawala wa kidikteta.
Hamadi Jebali ambaye pia ni mmoja wa viongozi wa zamani wa chama cha al Nahdha cha Tunisia ameishutumu vikali Imarati kwa kufanya njama za kufelisha mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na kumuua kigaidi Shukri Blayid, mmoja wa viongozi wa upinzani nchini humo mwaka 2013.
Amegusia pia namna Umoja wa Falme za Kiarabu unavyomwaga fedha nyingi za kuvuruga demokrasia huko Tunisia na kufelisha mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo akisisitiza kuwa, Imarati inahusika pia katika kufanya uharibifu kwenye nchi nyingine za Kiarabu za Syria, Yemen na Libya.
Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Tunisia amefafanua kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu unapinga mambo yenye thamani kama uhuru, mabadiliko na mapinduzi ya nchi yoyote ile na hufanya njama mbalimbali za kufelisha mambo hayo ya kimisingi katika maisha ya wanadamu.
Itakumbukwa kuwa rais wa zamani wa Tunisia, al Mansouf al Marzouqi, mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuwa, Umoja wa Falnme za Kiarabu unayasaidia magenge yanayopinga mapinduzi ya wananchi huko Tunisia kwa lengo la kukabiliana na harakati za kimapinduzi kwani ina hofu kuwa harakati hizo zikipata nguvu katika ulimwengu wa Kiarabu, tawala za kikoo na kifalme kama Imarati zitakuwa hatarini.