Makomandoo wa Uingereza wajeruhiwa na vikosi vya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i52368-makomandoo_wa_uingereza_wajeruhiwa_na_vikosi_vya_yemen
Duru mpya za habari zimefichua kuwa, makomandoo kadhaa wa Uingereza wamejeruhiwa katika makabiliano ya ana kwa ana na vikosi vya Yemen, na hivyo kuweka bayana kuwa serikali ya London imekuwa ikishiriki moja kwa moja katika vita vya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Mar 24, 2019 03:27 UTC
  • Makomandoo wa Uingereza wajeruhiwa na vikosi vya Yemen

Duru mpya za habari zimefichua kuwa, makomandoo kadhaa wa Uingereza wamejeruhiwa katika makabiliano ya ana kwa ana na vikosi vya Yemen, na hivyo kuweka bayana kuwa serikali ya London imekuwa ikishiriki moja kwa moja katika vita vya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Gazeti la The Mail la Uingereza limefichua leo Jumapili kuwa, makomandoo watano wa kikosi maalumu cha kijeshi cha Uingereza kinachofahamika kama Special Boat Service (SBS) wamejeruhiwa kwa risasi baada ya makabiliano makali kati yao na wapiganaji wa Ansarullah katika mkoa wa Saada wa kaskazini mwa Yemen.

Habari zaidi zinasema kuwa, makomandoo hao wamepata majeraha ya risasi katika sehemu tofauti za miili yao ikiwemo mikono na miguu, na kwamba baadhi yao wamerejeshwa nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu zaidi.

Inaarifiwa kuwa, karibu maafisa 30 wa kikosi maalumu cha kijeshi cha Uingereza cha SBS wamekita kambi katika maeneo ya mkoa wa Saada, wakiwemo madaktari, wakalimani, na wataalamu wa kudhibiti ndege za kijeshi almaarufu Forward Air Controllers (FACs), wenye jukumu la kuongoza ndege za kivita za Saudia nchini Yemen. 

Makao makuu ya kikosi cha Special Boat Service (SBS) cha Uingereza yapo Poole, mjini Dorset na kina makomandoo 200  

Kwa mujibu wa Vuguvugu la Kupambana na Biashara ya Silaha nchini Uingereza, tangu mwanzoni mwa mgogoro wa Yemen mnamo Machi mwaka 2015, UK imeiuzia Saudi Arabia silaha zenye thamani ya pauni bilioni 4.7.

Vita vya Saudia na washirika wake nchini Yemen hadi sasa vimepelekea mauaji ya zaidi ya watu elfu 16, makumi ya maelfu kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Hata hivyo Saudia na washirika wake wameshindwa kabisa kufikia malengo yake haramu ndani ya nchi hiyo kutokana na muqawama wa Wayemen.