Amnesty yasema Bahrain inatumia mashindano ya magari kujikosha
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema Bahrain inaendelea kutumia mashindano ya magari ya Langalanga maarufu kama Formula 1 kwa ajili ya kujikosha.
Samah Hadid, Mkurugenzi wa Amnesty katika eneo la Asia Magharibi aliyasema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, utawala wa Manama unaokandamiza wananchi unataka kutumia mashindano yajayo ya Formula 1 (F1) kujaribu kusafisha sura yake iliyochafuliwa na rekodi mbaya ya kukanyaga haki za binadamu. Mashindano hayo yanatazamiwa kufanyika kati ya Ijumaa ijayo hadi Jumatatu katika mji mkuu Manama.
Amebainisha kuwa, "Badala ya kujikosha, serikali ya Bahrain inapaswa kutazama upya sheria zinazopiga marufuku uhuru wa kujieleza sambamba na kuanzisha mchakato wa kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa."
Mkurugenzi wa Amnesty International katika eneo la Asia Magharibi ameongeza kuwa, "Nyuma ya shamrashamra za F1, kuna upande wa pili wa kutisha nchini Bahrain. Dola ni kandamizi na yeyote anayeikosoa serikali hata kwenye Twitter tu, anafungwa jela."
Juzi Jumatano, wanaharakati wa haki za binadamu wakiwemo maafisa wa Human Rights Watch na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wafanyakazi, walisema ni kichekesho jamii ya kimataifa kuruhusu mashindano hayo ya kimataifa ya Grand Prix Formula One kufanyika nchini Bahrain, katika hali ambayo utawala wa Aal-Khalifa unaendelea kuwakandamiza wananchi.
Aprili mwaka jana, maafisa usalama wa Bahrain waliwashambulia wananchi waliokuwa wamemininika mabarabarani kushiriki maandamano ya amani ya kupinga kufanyika nchini humo mashindano hayo ya magari ya Formula 1, ambayo yamekuwa yakifanyika nchini humo tangu mwaka 2004, isipokuwa mwaka 2011. Waandamanaji kadhaa walijeruhiwa na wengine wengi kutiwa mbaroni.
Tarehe 14 Februari mwaka 2011 wananchi wa Bahrain walianzisha vuguvugu la mapambano kwa kufanya maandamano ya amani dhidi ya utawala dhalimu na kandamizi wa Aal Khalifa.