Ripoti: Saudia inawatesa Waislamu wa Myanmar inaowazuilia
Ripoti mpya imefichua kuwa Saudi Arabia inawatesa na kuwadhalilisha Waislamu wa Kirohingya wanaozuiliwa katika jela ya utawala huo wa kifalme.
Ripoti ya shirika la habari la Middle East Eye imeeleza bayana kwamba, watawala wa Riyadh wanawapa mateso makali Warohingya hao wapatao 650, ili kuwalazimisha wasitishe mgomo wao wa kula.
Ripoti hiyo imefafanua kuwa, wakimbizi hao wa Kirohingya wanaozuiliwa katika jela ya Shumaisi magharibi mwa mji bandari wa Jiddah nchinin Saudia wanakabiliwa na kila aina ya mateso, kwa lengo la kuwataka wasitishe mara moja mgomo wao wa kususia chakula.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Middle East Eye, aghalabu ya Waislamu hao wa jamii ya Rohingya wanaozuiliwa nchini Saudia wamekumbwa na matatizo ya kisaikolojia, kwa kufungwa na kuteswa kwa muda mrefu, baadhi yao wakiwa kizuizini tangu mwaka 2012.
Itakumbukwa kuwa, mapema mwaka huu Saudi Arabia iliwasafirisha kwa nguvu hadi nchini Bangladesh makumi ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya waliotorokea nchini humo baada ya kushadidi mauaji na mashambulizi dhidi yao katika nchi yao ya Myanmar.
Maelfu ya Waislamu wameuawa na wengine zaidi ya milioni moja wamelazimishwa kuwa wakimbizi ndani na nje ya Myanmar kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na jeshi la nchi hiyo likishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali.