Jul 07, 2019 11:40 UTC
  • Wapalestina wataka umoja wa kitaifa ili kukabiliana na mpango wa 'Muamala wa Karne'

Viongozi wa harakati za mapambano ya Palestina wamesisitiza juu ya udharura wa kuweko umoja wa kitaifa huko Palestina ili kukabiliana na mpango uliojaa njama wa Muamala wa Karne.

Wakizungumza huko Beirut mji mkuu wa Lebanon viongozi hao wameashiria ulazima wa Wapalestina wote kusimama na kukabiliana na mpango wa Muamala wa Karne na kuwapongeza wananchi wa baadhi ya mataifa ya Kiarabu kwa kufanya juhudi za kuupinga mpango huo unaopigiwa upatu na Marekani. 

Aidha wamesema bayana kwamba, ili kukabiliana na mpango huo mchafu wa Muamala wa Karne kuna haja ya kupatikana umoja wa kitaifa miongoni mwa Wapalestina.

Maanadamano ya kupinga mpango wa 'Muamala wa Karne'

Itakumbukwa kuwa, kongamano la Bahrain la kuzindua mpango wa Muamala wa Karne lilifanyika tarehe 25 na 26 mwezi uliopita wa Juni huko Manama mji mkuu wa Bahrain.

Mkutano huo ulisusiwa na makundi yote ya Wapalestina, suala ambalo lilizusha maswali mengi juu ya uhalali wake na kuufanya upoteze maana na hivyo kugonga mwamba.

Mpango wa "Muamala wa Karne" ambao umebuniwa na Marekani kwa ajili ya kukandamiza kikamilifu kadhia ya Palestina unahimiza kutoruhusiwa wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi za mababu zao, kukabidhiwa mji wa Beitul-Muqaddas mikononi mwa utawala wa Kizayuni wa Israel, kuweko nchi ya Palestina lakini isiyo na jeshi wala nguvu zozote za uongozi na ukandamizaji mwingine mbalimbali dhidi ya taifa la Palestina.

Tags