Bintimfalme wa Saudia kuhukumiwa kifungo cha miezi sita Ufaransa
Mwendesha mashtaka mkuu wa Ufaransa ametaka kutolewa hukumu ya kifungo cha miezi sita jela na faini ya yuro elfu sita dhidi ya binti wa mfalme wa sasa wa Saudi Arabia kwa kupatikana na hatia ya kufanya ukatili dhidi ya mfanyakazi aliyekuwa akikarabati nyumba yake mjini Paris.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Ufaransa imetangaza kuwa, kesi ya Hassa binti Salman bin Abdul Aziz imefanyika bila ya yeye mwenyewe kuwepo mahakamani.
Amri ya kutiwa nguvuni binti wa Mfalme Salman wa Saudi Arabia ilitolewa Disemba mwaka 2017 kwa tuhuma za kushirikiana na mlinzi wake binafsi kufanya ukatili na kumdhalilisha mfanyakazi wake.
Mwaka 2016 Hassa binti Salman alimwamuru mlinzi wake binafsi kumpiga na kumdhalilisha fundi Ashraf Eid aliyekuwa akikarabati nyumba yake huko magharibi mwa jiji la Paris kwa eti kosa la kupiga picha ndani ya nyumba hiyo. Mfanyakazi huyo ameiambia mahakama ya Paris kwamba, aliwekwa katika mazingira mabaya kupita kiasi na kwamba wakati huo Binti wa Mfalme wa Saudia alikuwa akimwamuru mlinzi wake binafsi amuue mfanyakazi huyo.
Mahakama ya Paris inasema mlinzi binafsi wa Bintimfalme wa Saudia, Hassa binti Salman bin Abdul Aziz, alimfunga mikono na miguu mfanyakazi huyo na kumpiga akimdhalilisha. Vilevile alimlazimisha kubusu miguu ya bintimfalme wa Saudia.
Kikao kijacho cha kesi hiyo kitafanyika tarehe 12 Septemba.
Hii si mara ya kwanza kwa mahakama za Ufaransa kutoa hukumu dhidi ya wanafamilia wa wafalme wa Saudi Arabia. Mwezi Machi mwaka 2013 mahakama ya Ufaransa ilitoa hukumu ya kuzuiliwa mali na milki za Maha al Sudeiry, mke wa aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, Nayef bin Abdul-Aziz Al Saud kwa sababu ya kukwepa kulipa gharama za kuishi kwenye hoteli moja nchini humo.