Los Angeles Time: Saudia haina uwezo wa kushinda vita nchini Yemen
Gazeti la Los Angeles Time limekosoa uvamizi wa kijeshi uliofanywa na Saudi Arabia nchini Yemen na kueleza kwamba haitawezekana kwa utawala wa Aal Saud kushinda vita hivyo.
Gazeti hilo linalochapishwa nchini Marekani limeandika katika tahariri ya toleo lake la leo kwamba: Baada ya kupita zaidi ya miaka minne tangu Saudia na waitifaki wake walipotumia kila njia kuisambaratisha harakati ya Ansarullah ya Yemen katika vita vilivyosababisha vifo vya watu wapatao laki moja na kuisaidia serikali iliyojiuzulu kushika tena hatamu za udhibiti wa nchi, Saudi Arabia hadi sasa haijaweza kupata ushindi wowote.
Los Angeles Time limeongeza kuwa, Saudia inatumia majina mawili kwa ajili ya operesheni zake za kijeshi dhidi ya Yemen, ambazo ni operesheni ya "Tufani ya Maamuzi Makali", ambayo haijawa na ukali na operesheni ya "Kurejesha Tumaini" ambalo halijarudi.
Utawala wa Aal Saud na waitifaki wake ikiwemo Imarati wameshindwa kufikia lengo lao la kuihami serikali ya vibaraka wao kutokana na muqawama na ungangari wa wananchi wa Yemen, na hivi sasa vibaraka na mamluki wa Imarati na Saudia wanapigana na kuuana wenyewe kwa wenyewe huko Aden kusini mwa Yemen.
Mapigano kati ya vikosi vya baraza la mpito la kusini lenye mfungamano na Imarati na vile vilivyo tiifu kwa Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa Yemen aliyejiuzulu, ambavyo vinaungwa mkono na Saudi Arabia yameshtadi tangu tarehe mosi ya mwezi huu wa Agosti huko mjini Aden.
Mamia ya familia za Wayemeni zimenasa kwenye mzingiro kutokana na mapigano hayo.
Tangu baada ya kuanzisha uvamizi na mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015, Saudia na Imarati kila moja imekuwa ikidhibiti baadhi ya maeneo ya ardhi ya nchi hiyo na kuwatumia vibaraka na mamluki wao kwa ajili ya operesheni za kijeshi dhidi ya vikosi vya Yemen.../