Oct 19, 2019 13:36 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah: Maadui wamejawa hofu kwa kushuhudia matembezi ya Arubaini

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah amesisitiza kuwa, uwepo wa mamilioni ya watu mjini Karbala ni jambo lisilo na mfano katika historia na kwamba Marekani, utawala haramu wa Kizayuni, mabeberu na madhalimu wa dunia wanahisi hofu kubwa kwa kushuhudia matembezi ya mamilioni ya watu katika Arubaini ya Imam Hussein (as).

Sayyid Hassan Nasrullah ameyasema hayo leo katika mji wa Baalbek kwa mnasaba wa marasimu ya Arubaini ya kuuawa shahidi Imam Hussein na kuongeza kuwa, uwepo wa mamilioni ya watu katika marasimu hayo hauna mfanano duniani ambapo watu kutoka maeneo yote ya dunia ikiwemo Ulaya na Marekani wamefika Karbala kwa lengo hilo. Ameongeza kuwa matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (as) kwa mara nyingine yamewadhihirishia wazi walimwengu hamasa ya mjukuu huyo wa Mtume. Kadhalika Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon sambamba na kuashiria matukio ya hivi karibuni nchini Lebanon amesema kuwa, baadhi ya viongozi serikalini na katika makundi ya kisiasa wanataka kukwepa majukumu yao na kujiweka kando sambamba na kuwatwisha wengine matukio ya sasa, suala linaloonyesha kutokuwepo mshikamano wa kitaifa na kutojali matukufu ya kiakhlaqi na kibinaadamu katika kushughulikia mustakbali wa wananchi.

Matembezi ya mamilioni ya watu katika marasimu ya Arubaini ya Imam Hussein (as) yanawatia hofu mabeberu wa dunia

Sayyidi Hassan Nasrullah amesema kuwa, ni lazima Walebanon washirikiane ili kuboresha uchumi na hali ya wananchi. Ameongeza kuwa mambo kama vile kutaka kufanyike uchaguzi wa bunge wa kabla ya wakati na kuundwa serikali mpya ni yenye kupoteza muda na kwamba serikali ya sasa ni lazima iendeleze shughuli zake kwa utaratibu mpya sambamba na kupata ibra kutokana na malalamiko ya hivi karibuni ya wananchi. Aidha Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amewahutubu waandamanaji kwa kusema kwamba, Hizbullah inaheshimu sauti na malalamiko yao hivyo muqawama, hautaiacha nchi na taifa la Lebanon kama ambavyo hautaruhusu Lebanon ipate madhara. Amesisitiza kuwa iwapo Hizbullah itaingia barabarani basi hakutakuwa na njia ya kurejea nyuma ghairi ya kufikiwa matakwa ya wananchi.

Tags