Picha za satalaiti zathibitisha; Marekani inafanya magendo ya mafuta ya Syria
Russia imesema picha za satalaiti zimetoa ithibati kuwa Marekani inafanya magendo ya mafuta ya Syria chini ya ulinzi wa vikosi vyake vya usalama.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia, Meja Jenerali Igor Konashenkov amesema leo Jumamosi kuwa, "Idara ya Intelijensia ya Anga za Mbali imetoa picha zinazothibitisha kuwa, mafuta yamekuwa yakihamishwa kwa kiwango kikubwa na kupelekwa kusafishwa nje ya Syria, chini ya ulinzi kamili wa vikosi vya Marekani."
Ameongeza kuwa, misafara ya magari yanayobeba mafuta hayo yanayosafirishwa nje ya Syria imekuwa ikilindwa na vikosi maalumu na mashirika binafsi ya kijeshi ya Marekani, na magendo hayo yamekuwa yakifanyika kabla na hata baada ya kushindwa genge la kigaidi na la Daesh (ISIS) nchini Syria.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia amenukuliwa na shirika la habari la TASS akisema kuwa, "Kwa kuzingatia kuwa pipa moja la mafuta ya Syria ni dola 38, mapato ya biashara hiyo ya kibinafsi ni zaidi ya dola milioni 30 kwa mwezi."
Haya yanajiri siku chache baada ya Mark Esper Waziri wa Ulinzi wa Marekani kusema kuwa mamia ya wanajeshi wa nchi hiyo wataondolewa Syria na kupelekwa nchini Iraq.
Hata hivyo Alkhamisi iliyopita, Rais Donald Trump aliidhinisha ombi la Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) la kubakisha wanajeshi 500 na zana za kijeshi za nchi hiyo kaskazini mashariki mwa Syria eti kwa lengo la kulinda visima vya mafuta vya nchi hiyo ya Kiarabu.