Putin: Tunataraji vita vitamalizika mwakani 2020 nchini Syria
-
Vladimir Putin
Rais Vladimir Putin wa Russia amemtumia salamu rais mwenzake wa Syria na kusema kuwa, ana matumaini mwaka 2020 (unaoanza kesho Jumatano) utakuwa wa kumalizwa vita nchini Syria na kupatikana usalama na utulivu katika maeneo yote ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la TASS, serikali ya Russia imetoa salamu maalumu za Rais Vladimir Putin kwa mnasaba wa kuwadia mwaka mpya wa 2020 na kusema kuwa rais huyo anatumai kwamba, 2020 utakuwa mwaka wa kumalizwa vita kikamilifu nchini Syria.
Taarifa hiyo hiyo imemlenga moja kwa moja Rais Bashar al Assad wa Syria na kwa mara nyingine Moscow imesema iko pamoja na wananchi na serikali ya Damascus na iko tayari kustawisha zaidi na zaidi uhusiano wa pande mbili katika nyuga zote.
Taarifa hiyo ya serikali ya Russia imehimiza pia wajibu wa kuheshimiwa na kulindwa umoja wa ardhi yote ya Syria.
Salamu hizo za mwaka mpya za rais wa Russia kwa rais wa Syria zimetolewa hivi sasa ambapo Msemaji wa Ikulu ya Russia, Dmitry Sergeyevich Peskov jana Jumatatu aligusia mashambulizi ya anga ya Jumapili usiku yaliyofanywa na droni za Marekani katika mpaka wa Syria na Iraq dhidi ya maeneo ya vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Iraq vya al Hashd al Shaabi na kusema kuwa, mashambulizi kama hayo hayakubaliki kabisa.
Msemaji huyo wa Ikulu ya Russia (Kremlin) ameongeza kuwa, hatua yoyote ya kuangamiza magenge ya kigaidi inakubalika, lakini kitendo chochote cha kushambulia vikosi vya kujitolea vya wananchi na kuhatarisha usalama wa nchi nyingine hakikubaliki kabisa.