Jan 01, 2020 07:57 UTC
  • Marekani kutuma askari 4000 Asia Magharibi baada ya ubalozi wake 'kuvamiwa' Iraq

Serikali ya Washington inajiandaa kutuma wanajeshi 4,000 wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, baada ya wananchi waliokuwa na ghadhabu wa Iraq kufanya maandamano mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad.

Maafisa watatu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) wamefichua kuwa, Kikosi cha 82 cha Anga cha Marekani kimewaweka tayari wanajeshi 4,000 wa nchi hiyo kwa ajili ya kutumwa katika eneo la Asia Magharibi ndani ya siku chache zijazo.

Maafisa hao wa Pentagon wameiambia kanali ya televisheni ya Fox News kuwa, kwa akali wanajeshi 500 wa miavuli wa US wapo njiani kuelekea nchini Kuwait.

Mapema jana, Mark Esper, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alisema jeshi la nchi hiyo litatuma askari 750 nchini Iraq kwenda kulinda maafisa na mali za ubalozi wa Washington jijini Baghdad.

Hapo jana, Wairaqi waliandamana mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad baada ya mazishi ya wapiganaji wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi ya Hashd al Shaabi waliouawa katika hujuma za anga za Marekani, ambapo walilaani vikali mashambulizi hayo dhidi ya vituo vya harakati hiyo, huku wakitaka wanajeshi wa US wafukuzwe nchini humo.

Maandamano ya Wairaqi katika ubalozi wa US mjini Baghdad

Wananchi wenye hasira wa Iraq waliteketeza moto lango la kuingia katika ubalozi huo wa Marekani mjini Baghdad na kupanda juu ya ukuta wa ubalozi huo na kutundika hapo bendera ya Hashdu Shaabi, huku wakipiga nara za 'Mauti kwa Marekani'.

Viongozi wa kisiasa na kidini wa Iraq na nchi nyingine duniani wamelaani vikali shambulizi hilo la anga la Marekani lililoua wapiganaji 25 wa Hashdu Shaabbi katika mkoa wa al-Anbar na kulitaja kuwa ukiukaji wa haki ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.

 

Tags