Hizbullah: Tumejiandaa barabara kuzima uchokozi wowote wa Israel
Afisa mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema harakati hiyo ya muqawama imejiandaa vilivyo na ipo tayari kikamilifu kukabiliana na uvamizi na chokochoko zozote za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sayyid Hashem Safieddine, Mkuu wa Baraza Kuu la Utendaji la Hizbullah amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon na kueleza bayana kuwa, "harakati ya muqawama imejiandaa vilivyo na tumekwishaainisha machaguo ya kuchukua iwapo tutajikuta katika makabiliano na maadui."
Hata hivyo amesisitiza kuwa, harakati hiyo ya Kiislamu haifuatilii vita na wala haitaki kuchochea vita, lakini imejiandaa barabara kuzima uchokozi wowote wa maadui.
Kadhalika Sayyid Hashem Safieddine ameashiria kuhusu kadhia ya Palestina na kubainisha kuwa, "ukombozi wa Quds Tukufu toka mikononi mwa Wazayuni maghasibu ni katika ajenda kuu za harakati za muqawama katika eneo."
Aidha Mkuu wa Baraza Kuu la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amekumbusha kuwa, jeshi la Israel litaendelea kushindwa na kukabiliwa na vipigo kama lilivyoshindwa na harakati za muqawama miaka ya nyuma katika eneo hili la Asia Magharibi, vikiwemo vipigo vikali lilivyopokea katika vita lilivyoanzisha mwaka 2000 na 2006 dhidi ya Lebanon.
Hali kadhalika amesisitizia umuhimu wa kuadhimishwa na kubakia katika nyoyo za ulimwengu wa Kiislamu Siku ya Kimataifa ya Quds, ambayo huadhimishwa kote duniani Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kila mwaka.