Israel kujenga 'vitongoji 300 vya Trump' katika Milima ya Golan, Syria
Utawala ghasibu wa Israel unapanga kujenga mamia ya vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni katika Miinuko ya Golan nchini Syria, vitakavyoitwa "Miinuko ya Trump".
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa utawala huo wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, vitongoji hivyo vipya haramu katika ardhi ya Syria vitapewa jina la Kiyahudi la "Ramat Trump" linalomaanisha "Milima ya Trump".
Netanyahu amesema hayo katika kikao cha kila wiki cha Baraza la Mawaziri la utawala huo haramu na kuongeza kuwa, utawala huo pandikizi utajenga vitongoji 300 vya walowezi wa Kizayuni katika mpango huo.
Baada ya kikao hicho, Baraza la Mawaziri la Israel limetoa taarifa na kusema kuwa, "mpango huo wa kuviita vitongoji vipya katika Miinuko ya Golan kwa jina la Trump ni kuonyesha shukrani zetu za dhati kwa rais wa Marekani kwa kazi yake."
Baraza hilo limepasisha bajeti ya dola milioni 2.3 kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa vitongoji hivyo kinyume cha sheria katika ardhi ya Syria.
Itakumbukwa kuwa, Machi mwaka jana 2019, Trump alidai kuwa Milima ya Golan ya Syria ni mali ya utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo akatangaza kulitambua rasmi jambo hilo.
Katika kujibu hatua hiyo ya kichokozi ya Trump, serikali ya Damascus ilisema kuwa kitendo hicho ni sawa na kuishambulia moja kwa moja ardhi ya Syria kwani Milima ya Golan ni sehemu isiyotenganishika na ardhi nyingine za nchi hiyo ya Kiarabu.