Jun 15, 2020 15:10 UTC
  • UN: Athari za corona kuua watoto 50,000 Afrika Kaskazini na Asia Magharibi

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, yumkini athari za ugonjwa wa COVID-19 zikaua makumi ya maelfu ya watoto katika nchi za kaskazini mwa Afrika na Asia Magharibi.

Indhari hiyo imetolewa katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo Jumatatu na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) katika mji mkuu wa Jordan, Amman.

Taarifa hiyo imesema taathira za moja kwa moja na sisizo za moja kwa moja za janga la corona huenda zikaua watoto 51,000 wenye chini ya umri wa miaka mitano katika maene0 hayo kufikia mwishoni mwa mwaka huu 2020.

WHO na Unicef zimesema kuwa, "katika hali ambayo hakujaripotiwa kesi nyingi za watoto kukumbwa na ugonjwa wa COVID-19 katika eneo hilo, ni wazi kuwa janga hilo (la corona) limekuwa na taathira kwa afya za watoto hao."

Taasisi mbili hizo za UN zimetoa mwito kwa mifumo ya afya katika maeneo hayo kuchukua hatua za makusudi ili kuepusha kujitokeza senario hiyo ya kupoteza maisha makumi ya maelfu ya watoto.

Mfumo wa afya wa Yemen umeharibiwa sana na vita na mapigano

Taarifa hiyo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) imeongeza kuwa, "kuvurugwa utoaji wa huduma muhimu za afya na utapiamlo miongoni mwa watoto kunapunguza uwezekano wa kubakia hai watoto hao kwa miongo miwili."

Ugonjwa wa COVID-19 hadi sasa umeshaua watu zaidi ya 436,000 katika maeneo mbali mbali duniani, mbali na wengine zaidi ya 8,020,000 kuambukizwa virusi hatarishi vya corona.

 

 

Tags