Nasrullah: Mapambano ya Hizbullah hayaishii ndani ya mipaka ya Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i62973-nasrullah_mapambano_ya_hizbullah_hayaishii_ndani_ya_mipaka_ya_lebanon
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kutekeleza majukumu kwa ajili ya kuisaidia jamii yote ya wanadamu ni jambo la wajibu kwa mujibu wa thamani za Uislamu, na kwamba mipaka ya kijografia na kisiasa haipaswi kuwa kizingiti cha kutekeleza wajibu huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 23, 2020 03:20 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah
    Sayyid Hassan Nasrullah

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kutekeleza majukumu kwa ajili ya kuisaidia jamii yote ya wanadamu ni jambo la wajibu kwa mujibu wa thamani za Uislamu, na kwamba mipaka ya kijografia na kisiasa haipaswi kuwa kizingiti cha kutekeleza wajibu huo.

Sayyid Hassan Nasrullah aliyasema hayo katika hotuba yake ya jana Jumamosi kwa mnasaba wa kuwadia siku ya tatu ya Maombolezo ya Ashura ya Imam Hussein AS na kueleza bayana kuwa, Uislamu umewafaradhishia wafuasi wake kuwasaidia watu wenye mahitaji kwa kadri ya uwezo wao, na kwamba: Tunapaswa kutumia uwezo wetu wa kifedha na kijeshi kuwasaidia watu wengine bila kujali mipaka ya kikabila, kijografia na kisiasa.

Ameshangazwa na kuukosoa vikali undumakuwili wa Wamagharibi akihoji, "kwa nini uingiliaji wa kijeshi na kisiasa wa Marekani unakubalika katika aghalabu ya nchi duniani lakini usaidizi na uungaji mkono wa Hizbullah kwa nchi waitifaki katika eneo haukubaliki?" 

Sayyid Nasrullah amekumbusha kuwa: Imam Hussein AS angeliweza kukwepa jukumu lake la kidini kwa kujiepusha na makabiliano yaliyopelekea auawe shahidi, lakini Mjukuu huyo wa Mtume SAW alichagua njia ya kuunusuru Uislamu kuondokana na ufisadi wa Yazid.

Wanamapambano wa Hizbullah

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, harakati hiyo ya muqawama itaendelea kupambana na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) katika nchi za Syria na Iraq, ili kulifanya lisipanua satua yake katika nchi nyingine za eneo la Asia Magharibi.

Hali kadhalika amebainisha kuwa, Hizbullah itaendelea kuunga mkono mapambano ya Wapalestina katika hali zote, na kwamba harakati hiyo ya muqawama itawalinda wananchi wa Lebanon dhidi ya hatari ya magenge ya kitakafiri.